
KUTAMBUA
alama za nyakati na kuangalia maisha yako ni jambo la msingi sana
rafiki zangu. Kwa majuma matatu mfululizo yaliyopita, tumeona alama
nyingi za wenzi ambao siyo sahihi kutokana na tabia zao.

Tulianza
kwa kuwaangalia wanawake, tukaingia kwa wanaume ambapo tunaendelea pale
tulipoishia kabla ya kugeukia katika ushauri kwa wote. Wiki iliyopita
tuliishia pale ambapo mwanamke humshusha mwanaume waziwazi kwa matendo
yake.
Mfano kusifia wanaume wengine mbele ya mwenzi wake au kufanya jambo
lolote linaloashiria kuwa yupo naye lakini si kwa malengo ya muda mrefu.
Hebu sasa tuendelee kujifunza...
HATAOLEWA NA WEWE!Mwanamke huyu anaweza
kuzungumzia kuhusu kuolewa lakini siyo na wewe. Mathalani, anaweza
kusema: “Duh! Mwanaume atakayenioa atakuwa na kazi sana.”
Kauli hiyo ni tata na mara zote haina maelezo mengine yoyote mbele yake.
Ni kweli anajua kwamba ataolewa siku moja, lakini wewe huna chako.
Anamuwaza mwanaume mwingine kabisa. Hata hivyo, hawezi kukuambia
mojamoja, atatumia tenzi, ngano na methali katika kufikisha ujumbe huu
kwako.
MASHARTI KIBAOMwanamke huyu ni mjanja sana,
anaonekana ana mambo mengi, ni kama hataki mapenzi yajulikane, lakini
mbaya zaidi kwa kuwa anajua wazi kwamba hana mapenzi na wewe hataki
umharibie!
Ana masharti kibao ambayo hayaeleweki. Hapendi muongozane,
hasa kwenye sehemu zenye watu wengi. Hata kama ikilazimika kufanya
hivyo, hukuchagulia mahali pa kupita.
HANA WIVU...Hafikirii sana kuhusu kusalitiwa,
hana muda na simu yako na wala haonyeshi dalili zozote za kujali sana
penzi lako. Hafikirii kwamba siku moja unaweza kumsaliti. Hana muda huo.
Anaweza kukudhihirishia hili moja kwa moja, hata pale utakapokuwa
umepanga kutoka naye, halafu ghafla akakuambia amepata dharura lakini
atakupa rafiki yake uende naye kwenye pati. Hili ni tatizo na ni lazima
uwe nalo makini kwa kiwango cha mwisho.
Mwanamke ambaye hana wivu, kuna mapenzi kweli hapo? Hana shida na
wewe ndiyo maana basi hafikirii sana kuibiwa. Iache akili yako itafakari
hili kwa makini, mwisho wa siku utajua cha kufanya.
RATIBA ZISIZOELEWEKA Ana mambo mengi sana ambayo
hayaeleweki, pengine ana ratiba zake kabisa, lakini hakuweki! Yeye
anawaza mipango yake kama yeye na inawezekana kabisa hujui ratiba zake
na hajakuambia.
Hata kama alikuambia, siyo ratiba yake kamili. Kimsingi hataki
ufahamu kabisa juu ya mambo yake. Hii nayo ni alama tosha ambayo
itakufanya uelewe kwamba upo katika penzi la wizi. Hakuna anayekupenda
hapo.
USHAURI KWA WOTEMapenzi siyo kitu cha mchezo,
umakini ni jambo la kwanza kabisa ambalo unatakiwa kuwa nalo katika
uhusiano. Siku zinazidi kwenda mbele, sasa hakuna sababu ya kuendelea
kupoteza muda kwa mtu ambaye umeshagundua kuwa hakupendi.
Hana ‘future’ na wewe, hawazi kwamba unaweza kuwa wake wa maisha siku
moja, wakati wewe ukiwaza hayo, mwenzako anawaza mambo mengine. Upo
naye kwa ajili ya mapenzi ya dhati, mwenzio yupo kwa sababu ya kustarehe
tu.
Tafakari kwa makini, lakini kuna sifa zaidi za kuziangalia ili kuona
kama mwenzi uliyenaye ni kweli anafaa kuwa wako wa maisha au unapoteza
muda wako. Hata kama anakupenda lazima uwe na sababu zako za kumfanya
awe wako wa maisha.
Mambo yafuatayo ni muhimu zaidi kuzingatia wakati ukiwa katika
uhusiano ambao unahitaji uwe wenye malengo. Tuendelee kujifunza...
NI WA NDOTO ZAKO?Jambo kubwa kuliko yote ambalo
unatakiwa kuliangalia kwa jicho la tatu ni kama mwenzi huyo ni wa ndoto
zako. Je, yukoje? Siku zote kabla ya kuamua kufanya chochote lazima
ujiulize kama ndicho ulichokuwa ukikifikiria.
Hata kwa upande wa mwenzi wako, lazima ujiridhishe, ni kweli ni yule
uliyekuwa unamtarajia? Ana sifa unazohitaji? Acha tabia ya kujifariji
kwamba utampenda taratibu ndani ya ndoa, hicho kitu hakipo.
Hakuna kujifunza kupenda katika ndoa, lazima ujihakikishie mwenyewe
kuwa mwenzi wako ni yule mwenye sifa ulizokuwa ukizitarajia. Hili ni la
msingi, maana unaweza kuwa naye siku mbili, ukatamani mwingine nje. Kwa
nini? Kwa sababu si yule mwenye sifa ulizotarajia.