Wednesday, January 22, 2014

ANGALIA ALAMA HIZI, ANZA MWAKA NA FIKRA MPYA!-4

KUTAMBUA alama za nyakati na kuangalia maisha yako ni jambo la msingi sana rafiki zangu. Kwa majuma matatu mfululizo yaliyopita, tumeona alama nyingi za wenzi ambao siyo sahihi kutokana na tabia zao.
Tulianza kwa kuwaangalia wanawake, tukaingia kwa wanaume ambapo tunaendelea pale tulipoishia kabla ya kugeukia katika ushauri kwa wote. Wiki iliyopita tuliishia pale ambapo mwanamke humshusha mwanaume waziwazi kwa matendo yake.
Mfano kusifia wanaume wengine mbele ya mwenzi wake au kufanya jambo lolote linaloashiria kuwa yupo naye lakini si kwa malengo ya muda mrefu.
Hebu sasa tuendelee kujifunza...
HATAOLEWA NA WEWE!
Mwanamke huyu anaweza kuzungumzia kuhusu kuolewa lakini siyo na wewe. Mathalani, anaweza kusema: “Duh! Mwanaume atakayenioa atakuwa na kazi sana.”
Kauli hiyo ni tata na mara zote haina maelezo mengine yoyote mbele yake.
Ni kweli anajua kwamba ataolewa siku moja, lakini wewe huna chako. Anamuwaza mwanaume mwingine kabisa. Hata hivyo, hawezi kukuambia mojamoja, atatumia tenzi, ngano na methali katika kufikisha ujumbe huu kwako.
MASHARTI KIBAO
Mwanamke huyu ni mjanja sana, anaonekana ana mambo mengi, ni kama hataki mapenzi yajulikane, lakini mbaya zaidi kwa kuwa anajua wazi kwamba hana mapenzi na wewe hataki umharibie!
Ana masharti kibao ambayo hayaeleweki. Hapendi muongozane, hasa kwenye sehemu zenye watu wengi. Hata kama ikilazimika kufanya hivyo, hukuchagulia mahali pa kupita.
HANA WIVU...
Hafikirii sana kuhusu kusalitiwa, hana muda na simu yako na wala haonyeshi dalili zozote za kujali sana penzi lako. Hafikirii kwamba siku moja unaweza kumsaliti. Hana muda huo.
Anaweza kukudhihirishia hili moja kwa moja, hata pale utakapokuwa umepanga kutoka naye, halafu ghafla akakuambia amepata dharura lakini atakupa rafiki yake uende naye kwenye pati. Hili ni tatizo na ni lazima uwe nalo makini kwa kiwango cha mwisho.
Mwanamke ambaye hana wivu, kuna mapenzi kweli hapo? Hana shida na wewe ndiyo maana basi hafikirii sana kuibiwa. Iache akili yako itafakari hili kwa makini, mwisho wa siku utajua cha kufanya.
RATIBA ZISIZOELEWEKA
Ana mambo mengi sana ambayo hayaeleweki, pengine ana ratiba zake kabisa, lakini hakuweki! Yeye anawaza mipango yake kama yeye na inawezekana kabisa hujui ratiba zake na hajakuambia.
Hata kama alikuambia, siyo ratiba yake kamili. Kimsingi hataki ufahamu kabisa juu ya mambo yake. Hii nayo ni alama tosha ambayo itakufanya uelewe kwamba upo katika penzi la wizi. Hakuna anayekupenda hapo.
USHAURI KWA WOTE
Mapenzi siyo kitu cha mchezo, umakini ni jambo la kwanza kabisa ambalo unatakiwa kuwa nalo katika uhusiano. Siku zinazidi kwenda mbele, sasa hakuna sababu ya kuendelea kupoteza muda kwa mtu ambaye umeshagundua kuwa hakupendi.
Hana ‘future’ na wewe, hawazi kwamba unaweza kuwa wake wa maisha siku moja, wakati wewe ukiwaza hayo, mwenzako anawaza mambo mengine. Upo naye kwa ajili ya mapenzi ya dhati, mwenzio yupo kwa sababu ya kustarehe tu.
Tafakari kwa makini, lakini kuna sifa zaidi za kuziangalia ili kuona kama mwenzi uliyenaye ni kweli anafaa kuwa wako wa maisha au unapoteza muda wako. Hata kama anakupenda lazima uwe na sababu zako za kumfanya awe wako wa maisha.
Mambo yafuatayo ni muhimu zaidi kuzingatia wakati ukiwa katika uhusiano ambao unahitaji uwe wenye malengo. Tuendelee kujifunza...
NI WA NDOTO ZAKO?
Jambo kubwa kuliko yote ambalo unatakiwa kuliangalia kwa jicho la tatu ni kama mwenzi huyo ni wa ndoto zako. Je, yukoje? Siku zote kabla ya kuamua kufanya chochote lazima ujiulize kama ndicho ulichokuwa ukikifikiria.
Hata kwa upande wa mwenzi wako, lazima ujiridhishe, ni kweli ni yule uliyekuwa unamtarajia? Ana sifa unazohitaji? Acha tabia ya kujifariji kwamba utampenda taratibu ndani ya ndoa, hicho kitu hakipo.
Hakuna kujifunza kupenda katika ndoa, lazima ujihakikishie mwenyewe kuwa mwenzi wako ni yule mwenye sifa ulizokuwa ukizitarajia. Hili ni la msingi, maana unaweza kuwa naye siku mbili, ukatamani mwingine nje. Kwa  nini? Kwa sababu si yule mwenye sifa ulizotarajia.

No comments:

Post a Comment