Na Hans Mloli
POINTI tatu katika mechi nne za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, zimemfanya Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic, akose usingizi.
Logarusic, raia wa Croatia, maarufu kama Loga, amesema kati ya pointi hizo 12, tatu ni zile dhidi ya Yanga na amekuwa akipiga hesabu atazipata vipi kwa kuwa wakikutana anatambua ‘patachimbika’.
Akizungumza na Championi Jumatano, Logarusic amesema anajua mechi dhidi ya Yanga itakuwa ngumu sana lakini anazihitaji pointi zao tatu.
“Ndiyo pointi za Yanga ni muhimu sana, lakini jumla pointi 12 za mzunguko wa pili ndiyo zinaninyima usingizi.
“Mechi dhidi ya Yanga, Coastal Union, Mtibwa Sugar na Azam FC. Najua itakuwa kazi ngumu kuzipata, lakini nazitaka, ni muhimu sana kwetu kimahesabu,” alisema Loga.
Katika timu nne anazozihofia, mbili kati ya hizo, Loga ameishacheza nazo katika mechi ambazo si za mashindano.
Loga alikutana na Yanga katika mechi ya Nani Mtani Jembe na kuifunga mabao 3-1 wakati alipocheza na Mtibwa Sugar katika mechi ya kirafiki, kikosi chake kililala bao 1-0.
Tangu aanze kuifundisha Simba, haijawahi kucheza na Azam FC wala Coastal Union ambayo imefunga safari hadi nchini Oman kujiandaa na Ligi Kuu Bara.
Iwapo Logarusic atafanikiwa kukusanya pointi hizo 12 za timu hizo vigogo, maana yake atakuwa katika nafasi ya kutwaa ubingwa.
Simba inafungua dimba la mzunguko wa pili Jumapili, wakati watani wao Yanga na vinara wa ligi hiyo watatangulia dimbani Jumamosi.
Kuhusiana na mechi ya Jumamosi, Loga ametabiri kwamba wapinzani wao Yanga watashinda kirahisi.
No comments:
Post a Comment