Tuesday, August 12, 2014

UNDANI KIBONDE ALIVYOTIWA MBARONI

Stori: Shakoor Jongo
WIKIENDI iliyopita haikuwa njema kwa mtangazaji Ephraim Kibonde baada ya kutupwa nyuma ya nondo katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar kwa msala wa kudaiwa kugonga gari na kutoa lugha ya matusi, Ijumaa Wikienda lina full stori.
Mtangazaji Ephraim Kibonde akidhibitiwa na Polisi wa usalama barabarani maeneo ya Mwenge.
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini cha habari ambacho kimeshuhudia sakata hilo mwanzo mwisho, ishu nzima ilianzia maeneo ya Makumbusho ambapo gari alilokuwa akilitumia Kibonde, liligonga kwa nyuma gari jingine na kisha kukimbia.
“Baada ya kugonga, Kibonde alirudi nyuma kisha kuanza kukimbia ambapo trafiki alitumia gari lililogongwa na Kibonde kumkimbiza,” kilimwaga data chanzo hicho.Chanzo hicho kilifafanua kuwa baada ya polisi kumkimbiza kwa saa kadhaa, walifanikiwa kumkamata maeneo ya Mwenge ambapo trafiki alipanda kwenye gari la Kibonde na kumuamuru arudi eneo la tukio lakini Kibonde hakuwa tayari kurudi ndipo alipoanza kukimbia tena, huku askari aliyemkamata akiwa ndani ya gari.
Ephraim Kibonde akiwa nyuma ya nondo katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam.
“Inaonekana kulitokea kutoelewana kati ya askari na Kibonde ndipo askari huyo alipowasiliana na wenzie kwa njia ya radio call ili wambananishe na alipofika Ubungo kwenye mataa wakamtaiti na kumpeleka kituoni, Oysterbay,” kilihitimisha chanzo chetu.
Baada ya kupata maelezo hayo, kachero wa Ijumaa Wikienda alitia timu katika kituo cha Oysterbay ili kutaka kujua mustakabali mzima wa ishu hiyo ambapo alimshuhudia Kibonde akiwa amesimama nyuma ya nondo huku akiwa anaimba ‘nyimbo’ anazozijua mwenyewe.
Mtangazaji huyo amefunguliwa kesi iliyopewa RB namba OB/RB/13806/20014 KUGONGA NA   LUGHA YA MATUSI.

JACK PATRICK AYEYUKA GEREZANI

Stori:  Shakoor Jongo
Nini kinaendelea? Video Queen wa Bongo anayeshikiliwa na jeshi la polisi nchini China kwa msala wa madai ya kukamatwa na madawa ya kulevya ‘unga’, Jacqueline Fitizpatrick Cliff ‘Jack Patrick’ anadaiwa kuyeyuka gerezani.
Video Queen wa Bongo, Jacqueline Fitizpatrick Cliff ‘Jack Patrick’.
Kwa mujibu wa ‘mtu wetu’ aliyeambatana na rafiki zake Jack kwenda kumuona gerezani, Macau, Hong Kong nchini humo, walijikuta wakipigwa na butwaa kuambiwa hakuna mtu kama huyo gerezani hapo hivyo kuibua hofu kuwa huenda amenyongwa.
Uchunguzi wetu gerezani hapo ulibaini kwamba tofauti na hofu ya rafiki zake, kuna uwezekano Jack amehamishiwa gereza lingine lililopo nje kidogo ya Mji wa Macau.Chanzo chetu hicho kilidai kwamba habari za ndani zilieleza kwamba Jack amehamishwa gereza hivyo kwa maelezo zaidi watu wanaokwenda kumtembelea waende kwenye ofisi za gereza hilo alilokuwa awali watapewa maelekezo wapi alipo mtu wao.
Jacqueline Fitizpatrick Cliff ‘Jack Patrick’ akiwa Chini ya ulinzi mkali China.
“Unajua watu wanaokwenda kumtembelea Jack gerezani ni Watanzania walioko huku China kwa shughuli maalum hasa za sanaa, kama vile sarakasi au maigizo, wengine wote wanaogopa, wanajua wanaweza kukamatwa.
“Tulipokwenda na mazagazaga yetu tuliambiwa Jack amehamishwa gereza na inaonekana aliomba mwenyewe ila hatujui ni kwa nini alifanya hivyo,” kilisema chanzo hicho.Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, John Haule alitoa taarifa na kutaja jumla ya watuhumiwa waliokamatwa kwa kesi za madawa ya kulevya ambapo alisema kuwa kuna Watanzania wengi wapo kwenye magereza mbalimbali China.
“Katika magereza ya China hadi Februari (mwaka huu) tulipewa taarifa kwamba wapo Watanzania 177 magerezani na kati ya hao 15 wamehukumiwa kunyongwa kutokana na baishara hiyo ya madawa ya kulevya,” ilisema taarifa hiyo ya katibu mkuu.
Jack alikamatwa Macau, Hong Kong, mwaka jana hivyo kesi yake inaendelea kuunguruma. Tofauti na Beijing ambao huwa wananyonga watu wanaojishughulisha na unga, Hong Kong ni kifungo cha miaka kadhaa tu.

ANAYEDAIWA KUMPA MIMBA MBWA KORTINI


Stori: Haruni Sanchawa na Makongoro Oging’
LILE sakata la mume aliyetajwa kwa jina la Hamis Juma (pichani akiwa na mkewe), mkazi  wa Majohe Mji Mpya, Ilala jijini Dar kudaiwa na mkewe, Cecilia Hamis kwamba amempa mimba  mbwa yameibuka mapya, Uwazi limeyanyaka.
Cecilia Hamis (kulia) akiwa na mume wake (mtuhumiwa) Hamis Juma.
Ijumaa iliyopita, Uwazi lilifika kwenye ofisi za Taasisi ya Kutetea Haki za Wanyama ambapo mmoja wa maofisa aliyedai si msemaji maalum, alisema wapo katika mchakato wa kufuatilia madai ya mke wa mtuhumiwa huyo kisha kumpandisha mahakamani kujibu mashitaka ya kumdhalilisha mnyama huyo.Mbwa anayedaiwa kupewa mimba na Bw. Hamis Juma.
“Sisi ishu yetu si kufuatilia kama kweli amempa mimba bali ni kujiridhisha kama kweli yule mzee ametembea na mbwa hilo linatosha kabisa kumfikisha kortini,” alisema afisa huyo na kuomba jina lake lisichapishwe gazetini.
WAGOMA MBWA KUUAWA
Jingine jipya lililotua Uwazi linadai kuwa, baadhi ya majirani wa nyumbani kwa Hamis wamegoma mbwa huyo kuuawa baada ya wengine kutaka kufanya hivyo wakisema hali hiyo itaweza kusababisha mdaiwa huyo kufanya matukio mengine nje ya nyumba yake.
MENGINE TENA
Katika hatua nyingine, Uwazi limebaini kuwa, kumbe mwanaume huyo ana sakata lingine ambapo ana kesi kwenye Mahakama ya Mwanzo Ukonga jijini Dar  akikabiliwa na tuhuma za kumfanyia fujo jirani yake.
Kwa mujibu wa taarifa za kimahakama, ilidaiwa kuwa Hamis alifika nyumbani kwa Alanus Haule ambaye ni jirani yake saa saba usiku wa siku ya tukio akiwa na  silaha za kienyeji na chepe akiwa amelewa na kuanza kumtolea maneno ya vitisho huku akijua ni kosa kisheria chini ya kifungu cha sheria 89 (1) B CAP 16.
Kesi hiyo yenye No 873/2014 ambayo inasikilizwa na Hakimu Mwandamizi, Raia Omary kwa mara ya mwisho ilisikilizwa Julai 3, mwaka huu na kuahirishwa hadi Septemba 11, mwaka huu na yuko nje kwa dhamana.
Habari hii kuhusu Hamis Juma kudaiwa kumpa mimba mbwa, kwa mara ya kwanza ilitoka katika gazeti hili toleo namba 854 la Agosti 5-11, 2014 ambapo kichwa cha habari kilisomeka ‘MUME WANGU KAMPA MIMBA MBWA.’

MPENZI WAKO AKIKUAMBIA MANENO HAYA, ZINDUKA! - 2

NINA furaha sana moyoni mwangu maana ninakwenda kuzungumza na wewe kuhusu mambo muhimu sana katika maisha yetu ya kimapenzi.
Rafiki zangu, nazungumza juu ya kauli ambazo zina ishara mbaya kwenye uhusiano. Wakati mwingine unaweza kumsikia mpenzi wako akikuambia maneno ya ajabu sana, lakini usielewe maana yake ni nini.
Ngoja nikuambie, kila kinachotoka kinywani mwa mpenzi wako kukuambia wewe kina maana yake. Lengo ni kujifunza; kufahamu maneno hayo na maana zake. Wiki iliyopita tulianza na maneno, huvutii na hupendezi. Sasa tuendelee.
UNATOA HARUFU...
Mwenzi ambaye hana mpango tena na wewe, ataanza kukuonea kinyaa. Maneno ya kejeli kwake si suala la kujiuliza mara mbili. Ni rahisi sana kukuambia unanuka!
“Ebwanae unanuka jasho sana, hebu kaoge kwanza,” anaweza kukuambia hivyo.
Katika hali ya kawaida kabisa hii ni dharau, ila inawezekana labda mpo katika hatua ya kuelekea kwenye mahaba, lakini ulipomsogezea kinywa chako, ukakutana na maneno haya: “Aaaah! Mh...unanuka mdomo bwana, sitaki!”
Hizi si kauli njema na bila shaka anajaribu kukuonesha jinsi ambavyo umepungua thamani kwake. Huwezi kunuka kwa mpenzi wako, siku zote huwa unanukia, lakini kama ameona dosari yoyote na yeye kama mwenzi wako wa karibu ana wajibu wa kuhakikisha anatumia lugha nzuri kukurekebisha, lakini kwa kuwa hana mapenzi na wewe, hana haja ya kuonesha mapenzi yake, anakubwatukia atakavyo!
KUHUSU NDOA
Wengi wanapokuwa katika uhusiano wanakuwa na ndoto zao, lakini ni aghalabu kukuta mtu yupo kwenye uhusiano wa kula raha tu! Mara nyingi ndoto kubwa huwa ni ndoa, ingawa ni vyema kupeana muda wa kuchunguzana kwa muda mrefu zaidi kabla ya kufikia azimio hilo muhimu maishani.
Lakini unapokuwa na mpenzi wako faragha, kwenye mazungumzo au katika matembezi ya jioni halafu ghafla akakuambia hana mpango wa kuoa au kukuoa, ni kama anakupa tiketi ya kukuacha.
Pima kauli hii, kama anazungumza kwa mzaha utagundua na kama yupo ‘serious’ pia utajua. Angalia macho yake na namna anavyoweka mkazo kwa kauli yake hiyo.
Lakini hata kama hatakuambia hana mpango wa kukuoa lakini kusema kwamba hana mpango wa kuoa kwa muda huu (huo) nayo ni alama kwamba hana ndoto ya kuendelea nawe tena na kama ataendelea, anapoteza muda tu.
HUWEZI MAHABA...
Hii ni mbaya zaidi maana inagusa eneo ambalo wengi hawapendi kuonekana hawawezi! Unaweza kuwa naye chumbani, ukijitahidi kadiri uwezavyo kuhakikisha anafurahia, lakini ghafla unashangaa anakuambia hujui mambo!
Tena wakati anakuambia, anatamka kwa kumaanisha huku akitaka uongeze ujuzi maana muda wote mliokuwa naye hapo, ni kama mlikuwa mnacheza!
“Jifunze ubunifu, kila siku huwa unaniacha kama nilivyokuja...nikueleze tu ukweli kwamba, hujawahi kukata kiu yangu hata siku moja!” Kwa kauli hii, hapo una mpenzi tena jamani?
Tafakari anachokuambia, kama kinaingia akilini au la. Kwa kawaida kama umekosea, anatakiwa kukushauri, siyo kukukashifu.

KAMA WEWE UMEJIFUNGUA SALAMA, MTOTO WAKO NI MZIMA MSHUKURU MUNGU


Makala Makongoro Oging’
DUNIANI kuna mengi kiasi kwamba kama mama  umebeba ujauzito kwa miezi tisa na kujifungua mtoto salama na mtoto wako ni mzima unapaswa kumshukuru Mungu kwani kuna watu ambao wanapata usingizi wa mang’amung’amu kutokana na mateso ya watoto wao.
Mtoto Godwin Florence Rweyemamu (3) akilia kwa maumivu anayoyapata.
Mtoto Godwin Florence Rweyemamu (3), mkazi wa Kijiji cha Kamala, Kata ya Bangwe mkoani Kigoma yupo ndani ya mateso makubwa yanayomfanya kulia muda wote kutokana na maumivu makali anayoyapata kwa ugonjwa wa kansa unaotafuna macho yake hivyo kumfanya asione.
HISTORIA YAKE
Akizungumza na Uwazi akiwa katika masikitiko makubwa
nyumbani kwa ndugu yake, Manzese jijini Dar, bibi wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Elda Charles Rweyemamu, mjukuu wake huyo alizaliwa akiwa hana tatizo lolote lakini alipofikisha umri wa miaka miwili na nusu akapatwa na ugonjwa wa mtoto wa jicho upande wa kushoto.
“Tuliamua kumpeleka kwenye Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni ambapo alitibwa akapata nafuu, tukarudi nyumbani.“Lakini wanasema ukizaliwa na balaa ni balaa tu, mwanzo hadi mwisho.
Mtoto Godwin Florence Rweyemamu (3) akiwa na bibi yake, Elda Charles Rweyemamu.
Kwani baada ya muda ugonjwa ulijirudia tena, sasa si mtoto wa jicho ila jicho likaonekana kuwa na uvimbe kidogo. Mimi na mama yake tulishangaa sana, tukaona lazima tuendelee kuhangaika. Tukampeleka katika Hospitali ya Matiazo.
“Madaktari walijitahidi, wakamtibu akapata nafuu tena na uvimbe katika jicho uliisha, tukajua tumeepukana na hilo.
UGONJWA WARUDI KWA KASI
Akiendeleza kusimulia mateso ya mtoto huyo, bibi huyo alisema:
“Baada ya kukaa kwa muda mfupi, ghafla ugonjwa ulirudi tena, sasa eti hata kichwa kilivimba. Hii hali ilitushangaza sana na tukawa tunaulizana ni nini?
“Nilimwambia mama yake kuwa Mungu ni wa kumtumaini muda wote, hivyo tukampeleka tena Hospitali ya Maweni lakini madaktari wakasema ili mjukuu wangu aendelee kuwa na uhai tuje hapa Muhimbili. Tulifunga safari ya kuja ambapo Julai 21, mwaka huu, tukawa tumefika.”
MATUMAINI YAREJEA, YAYEYUKA
“Tulipofika hapa Muhimbili na kuona hospitali yenyewe ilivyo kubwa na madaktari bingwa wengi niliamini kuwa mjukuu wangu angepona na kurudi naye nyumbani akiwa salama lakini cha kushangaza mambo yakawa tofauti na jinsi nilivyokuwa nikifikiria.
”Madaktari walimfanyia uchunguzi, baada ya siku nne waliniambia ugonjwa alio nao huyu mtoto ni kansa.
“Walinitoa machozi zaidi pale waliponiambia kuwa, hata hivyo hawataweza kumtibu kwa vile tulichelewa kumleta.”
“Lakini hata wao waliniambia wakiwa na masikitiko makubwa kwani nilishangaa kuwaona baadhi ya madaktari wakitoa machozi kwa kumuonea huruma mjukuu wangu kwa jinsi anavyolia muda wote kwa maumivu kama unavyomsikia,” alisema.
Aliongeza kuwa, walichofanya madaktari hao ni kumpa dawa ya kutuliza maumivu na kumwambia bibi mtu warudi nyumbani Kigoma kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa yote.
HANA NAMNA YA KURUDI KIGOMA
“Tangu nimeruhusiwa kutoka Muhimbili, Julai 26, mwaka huu sina jinsi ya kurudi nyumbani Kigoma. Nauli hadi kule ni shilingi 70,000. Kwa sasa nimepata hifadhi hapa Manzese kwa mdogo wangu ambaye anaishi kwa kufanya biashara ndogondogo lakini hana fedha. Kuendelea kukaa kwake ni sawa na kero kwani huyu mtoto amekuwa akilia mara kwa mara hali ambayo ni kero kwa wapangaji wenzake.
“Hata chakula ni tatizo, kila siku inabidi nimpeleke katika zahanati kusafisha macho. Kwa muda wa wiki moja nimetumia shilingi 300,000 kwani aliishiwa damu na inabidi aongezwe halafu kuna dawa za kutuliza maumivu aliongezewa, nina shida kubwa sana.”
KWA NINI BIBI NA MJUKUU?
“Kilichonifanya nije mimi huku Dar ni kwa vile mama yake ni mjamzito. Wakati wowote anaweza akajifungua. Pia ana mawazo mengi sana kwani watoto wake wawili, wa kwanza na wa pili walifariki dunia kutokana na magonjwa ya aina mbalimbali na huyu wa tatu ndiyo madaktari wamesema nimrudishe nyumbani tusuburi kifo,” alisema Elda kwa huzuniu
ANACHOOMBA
Anachoomba bibi huyo ni nauli ya kumuwezesha kurudi nyumbani kwake, Kigoma. Kwa aliyetayari anaweza kumsaidia kupitia namba  0762 175 117,
0784 420 215 au 0719 285 100.
Ndugu msomaji, kama ulivyosikia kilio cha bibi huyo ambaye yupo katika wakati mgumu wa kumuuguza mjukuu wake, hebu msaidie kwa chochote ulichonacho, tunaamini Mwenyezi Mungu atakubariki. Mhariri.

NI KWELI BILA UKAWA BUNGE LA KATIBA HALITAATHIRIKA?

Kikundi cha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Wakati vikao vya Bunge Maalum la Katiba vikiendelea tena mjini Dodoma wiki hii bila ya kuwepo kwa kikundi kinachojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samweli Sitta amesema amekuwa akisisitiza kuwa bunge hilo halitaahirisha shughuli zake hadi hapo muda wa siku 60 waliopewa utakapokamilika.
Sitta alisema rasimu hiyo ina mambo mengi mazuri lakini pia akasema kuna mambo mengine yanatakiwa kufanyiwa marekebisho ili Watanzania waweze kupata katiba bora.
Ni kweli kwamba maudhui ya rasimu ya katiba yanajumuisha baadhi ya mambo yafuatayo; kuimarisha Muungano wetu kwa kuleta uwiano bora wa mamlaka ya Zanzibar na Tanzania Bara ndani ya Muungano, kuimarisha haki za binadamu na kuzuia wachache kufuja rasilimali za taifa.
Naamini upo ukweli kwamba ndani ya rasimu hiyo inayojadiliwa yapo mapungufu kwa kuachwa masuala ya kuwezeshwa kuundwa kwa Serikali za Mitaa, maelekezo ya matumizi ya ardhi na rasilimali nyingine.
Hakika kitendo kinachofanywa na wajumbe wa bunge hilo wanaounda Ukawa ni kibaya kwani kususia kikao si jambo jema na badala yake wangelumbana kwa hoja ndani ya bunge.
Niwaombe tu wana Ukawa kwamba waache kupotosha umma na kuonekana kuwa wao ni bora zaidi ya wajumbe wengine walioko ndani ya Bunge Maalum la Katiba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Pandu Amir Kificho tayari amewasilisha mapendekezo ya kanuni 12 ambazo zitaliwezesha bunge hilo kukamilisha kazi yake katika muda uliopangwa wa siku 60.
Mapendekezo hayo yalipitishwa katika moja ya kikao cha jioni wiki iliyopita kwa kauli moja kutoka kwa wajumbe waliokuwepo na hivyo kazi ya kuanza kujadili sura zilizobaki zikaanza na zitaendelea wiki hii.
Kwa kumbukumbu zangu ni kwamba awali akichangia mapendekezo hayo, mjumbe wa bunge hilo na Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangala alisema kuundwe kanuni itakayowabana wajumbe waliotoka katika Bunge hilo na hata wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Sinde Warioba iliyoshughulikia mchakato wa ukusanyaji maoni kutoingilia mwenendo wa bunge hilo wakati huu vikao vyake vinapoendelea.
Ni jukumu la wapenda amani wote katika nchi hii kuwahimiza Ukawa kuingia katika meza ya maridhiano kwa sababu muda bado upo na ni vizuri sana wakaingia sasa bungeni kwa sababu yanayojadiliwa yanawagusa wananchi katika majimbo yao moja kwa moja.
Nizidi kumuomba Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe kuliona hili na kukumbuka wahenga waliosema kuwa hakuna vita inayokwisha nje ya meza ya mazungumzo. Hii ni hoja yangu, muitafakari tafadhali. Wanachi wote wanataka Katiba mpya itakayodumu miaka 50 ijayo.

WAPAKISTANI WA UNGA WATOROKA NCHINI!


Stori: Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
Wapakistani wawili, Abdul Ghan Peer Bux na Shahbaz Malk (pichani) waliokamatwa  wakiwa  na  Watanzania  wanaotuhumiwa kwa kukutwa  na  madawa ya kulevya wametoroka nchini.
 Mtuhumiwa Abdul Ghan Peer Bux.
Watuhumiwa hao walikamatwa Februari 21, 2011wakiwa na madawa ya kulevya yenye thamani ya  shilingi  bilioni 6.2,  Mbezi Beach  maeneo ya  Jogoo  jijini Dar sa Salaam.
Habari za uchunguzi ndani ya Mahakama Kuu zinasema kuwa, Jaji Grace Mwakipesile anayesikiliza kesi  hiyo  inayotarajiwa kuendelea kusikilizwa kesho Jumatano, ametoa amri ya kukamatwa  kwa  watuhumiwa  hao.
Kesi hiyo ambayo ilisikilizwa mahakamani hapo Julai 4, mwaka huu ilidaiwa kuwa Wapakistani hao walikamatwa  na  kikosi  kazi  cha  kuzuia na kupambana na madawa  ya kulevya kisha kudhaminiwa lakini wametoweka bila kuhudhuria mahakamani hata siku moja.
Mtuhumiwa Shahbaz Malk.
Imeelezwa kuwa, baada ya watuhumiwa hao kudhaminiwa na wadhimini wawili, Julai 4, mwaka mahakama iliambiwa kuwa wadhamini hao wamefariki dunia.
Hata hivyo, jaji anayesikiliza kesi hiyo aliwaagiza ndugu waliotoa taarifa hiyo kupeleka cheti halisi cha kifo kesho na watuhumiwa wahudhurie mahakamani  hapo.
Madawa ya kulevya yaliyokamatwa na watuhumiwa hao yenye thamani ya shilingi  bilioni 6.2.
Watanzania waliokamatwa na Wapakistani hao waliachiwa huru baada ya kulipa dhamana ya shilingi 10,000,000 ambapo wadhamini wao ni Raza Hussein Kanji ambaye alipewa stakabadhi namba 3406367 na Nazar Mohamed Nurd alikatiwa yenye namba 3406355.
Kamanda wa Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya nchini, Godfrey Nzowa.
Februari 21, 2011 polisi chini ya kamanda wao, Godfrey Nzowa waliwakamata Wapakistani hao wakiwa na Watanzania wawili, William Chonde na Kambi Zuberi ambao wapo nje kwa dhamana wakituhumiwa kukutwa na madawa ya kulevya yenye thamani ya shilingi bilioni 6.2.

BIBI KIZEE AJIANDALIA JENEZA!


Stori: Mwandishi Wetu, Songea
Mkazi wa Kijiji cha Lundusi, Kata ya Peramiho, wilayani Songea, Mkoa wa Ruvuma, Bibi Scholastica Mhagama amejiandalia jeneza lake ambalo litatumika kumzikia siku atakayoaga dunia.
Bibi Scholastica Mhagama(76) ambaye amejiandalia jeneza lake litakalotumika kumzikia.
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki iliyopita, Scholastica alisema alilitengeneza jeneza hilo zaidi ya miaka mitano iliyopita baada ya kuona anaishi kwa dhiki na anatengwa na baadhi ya watu.
“Nilijitengenezea jeneza langu na fundi alipomaliza kazi, niliingia ndani kupima kama ninatosha, nikajilaza na kuona liko sawasawa,” alisema bibi huyo.
Bibi Scholastica Mhagama akiliangalia jeneza lake.
Akifafanua zaidi bi mkubwa huyo alisema ameishi maisha ya dhiki na kunyanyaswa bila msaada kutoka kwa jamii anayoishi,  hali ambayo imemfanya amuombe Mungu amchukue ili azikwe kwenye jeneza alilojiandalia.
“Kila siku naomba Mwenyezi Mungu anichukue haraka ili nikapumzike kutokana na mateso ninayoyapata, lakini hofu yangu ilikuwa je nikifa, nitazikwa kama binadamu wengine? Ndiyo maana nimeamua kujiandalia jeneza langu,” alisema bibi huyo mwenye ulemavu wa mguu uliotokana na kung’atwa na nyoka kisha kukatwa huku mwingine ukimsumbua kukunjuka.
Bibi Scholastica Mhagama akiwa ndani ya nyumba anayoishi.
Alipoulizwa sababu ya kutengwa na jamii, bibi huyo alisema: “Nimetengwa na jamii na majirani wanashindwa kunisaidia wanadai eti mimi ni mchawi kwa sababu watoto wangu wote wanne walikufa wakiwa wadogo. Naumia sana kusingiziwa kitu ambacho sikijui.’’
Bibi huyo anayeishi katika kibanda kilichoezekwa kwa nyasi anasema kuwa, aliweza kutengeneza jeneza hilo baada ya kupewa shilingi 40,000 na mfadhili mmoja.
“Tayari nilikuwa na mbao, hivyo kazi ilikuwa kumlipa fundi fedha na kumpa mbao ili anitengenezee jeneza,” alisema Scholastica. Bibi Scholastica akiwa nje ya nyumba yake siku alipoongea na mwandishi wetu.

MAITI YA MBONGO YAWEKWA MOCHWARI CHINA MIEZI 8


Na Waandishi Wetu
VILIO, majonzi vilitawala katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Agosti 7, mwaka huu kufuatia kuwasili kwa mwili wa mwanafunzi wa kidato cha nne, Habiba Yusuph Ally (24) aliyefariki dunia kwa kubakwa nchini China miezi nane iliyopita.
Mwili wa Habiba Yusuph Ally (24) ukiwa katika jeneza eneo la uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Tukio hilo linaweka historia ya kusikitisha kwenye familia ya mzee Yusuph Ally kwa kuwa na msiba miezi nane wakati mwili wa binti yake ukiwa mochwari nchini humo baada ya kifo chake.
Habiba Yusuph Ally enzi za uhai wake.
KWA NINI MIEZI NANE?
Akizungumza na Uwazi kwa masikitiko makubwa, baba wa marehemu alisema kilichosababisha maiti ya binti yake ikae mochwari kwa muda wote huo ni utafutaji wa fedha kuwa mgumu lakini hatimaye Watanzania waishio nchini humo walifanikisha na kuuleta kwa ndege ya Shirika la Ndege la Emirates.
Mwili wa Habiba Yusuph Ally ukichukuliwa kutoka uwanja wa ndege.
ALICHOKIONA BABA CHAMSHTUA
Mara baada ya mwili huo kuwasili, kilifika kipengele cha kufunuliwa ili baba mzazi amtambue marehemu ambapo zoezi hilo lilimshtua mzee huyo kufuatia kuuona uso wa mwanaye ukiwa na majeraha kibao huku tumbo likiwa limeshonwa. Ilidaiwa ulifanyiwa uchunguzi.
MWILI WAPELEKWA NYUMBANI
Baada ya hapo, mwili huo ulipekekwa nyumbani kwa mzee Yusuph kwa ajili ya kuagwa na siku iliyofuata, Agosti 8, mwaka huu ukazikwa kwenye Makaburi ya Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam.
Mwili wa marehemu, Habiba Yusuph Ally ukipakiwa kwenye gari .
HABIBA ALIVYOKUFA
Katika gazeti ndugu na hili, Ijumaa Wikienda Toleo la Februari 24, mwaka huu liliandika habari ya kubakwa kwa Habiba hadi kufariki dunia. Habari hiyo ilikuwa na kichwa cha habari kilichosomeka; MBONGO ABAKWA CHINA, AFA! Kwa mujibu wa baba, Habiba alibakwa Januari 18, mwaka huu.
Maelezo ya habari hiyo yaliyotolewa na rafiki wa karibu wa Habiba aitwaye Saada yalisema siku ya tukio, marehemu alikutana na Mnigeria mmoja ambaye walipatana kulala wote kwa usiku mzima.
Alisema kumbe Mnaigeria huyo alikuwa na wenzake wanne. Usiku walimwingilia wote kwa nguvu mpaka akapoteza maisha palepale. Ulikuwa ukatili mkubwa.
Watu hao walipogundua Habiba amefariki dunia  waliuchukua mwili wake na kuutupa chini kutoka ghorofa ya tano walikokuwa wamempeleka kulala naye.
Baadhi ya waombolezaji wakiwa msibani.
Habari zaidi zilidai kuwa madaktari waliokuwa wakiuchunguza mwili wa Habiba waligundua haukuwa na figo na moyo jambo lililozidi kuzua hofu juu ya mauaji yake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mzee Yusuph juzi, Wanigeria hao walikamatwa na jeshi la polisi nchini humo na kufikishwa mahakamani kwa kudaiwa kuua.
Alisema mara baada ya kifo, polisi nchini humo waliizua maiti yake kwa muda ili kupisha upelelezi zaidi na baada ya kukamilika ndipo Watanzania walioko huko wakaanzisha mchango wa fedha kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania, China na kuusafirisha mwili wake.
MBONGO AONGEA
Uwazi lilibahatika kuzungumza kwa simu na Mtanzania anayeishi kwenye Mji wa Guangzhou nchini China (jina tunalo) ambaye alidai nguvu kubwa ilitumika kuchangishana fedha ili kuuleta Bongo mwili wa marehemu Habiba.
Masheikh wakiuswalia mwili wa Habiba kwa safari yake ya mwisho.
ATOA USHAURI
Mbongo huyo anayefanya biashara nchini humo alitoa ushauri kwa Watanzania wenye ndugu China kuwa makini nao kwa vile wengi wakifa, kama hakuna moyo wa kuchangiana huzikwa na taasisi zinazosimamia kazi hizo lakini ikibainika kuwa kuna michango inayoendelea, mwili unaweza kuwekwa mochwari hata miaka miwili.
HISTORIA YA MAREHEMU HABIBA
Marehemu Habiba aliondoka Bongo kwenda China mwaka 2010 akiwa na miaka 19 akisoma kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Kiluvya, Kinondoni, Dar kufuatia kurubuniwa na mwanamke mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Chausiku.
Vijana wakiushusha mwili wa Habiba kaburini.
Kwa mujibu wa baba wa marehemu, marehemu Habiba alikuwa mtoto wa tano kati ya saba, aliondoka nchini na mwanamke huyo bila kumwambia ndugu yeyote.
“Alirubuniwa na huyo Chausiku kwamba anakwenda kufanya kazi saluni lakini alipofika kule akamwingiza mwanangu kwenye biashara ya ukahaba. Hata hao waliombaka walimpata kwenye biashara hiyo,” alisema baba wa marehemu.
Wakati wa Mazishi ya Habiba.
Akaongeza: “Sisi tukiwa hatujui alipo, miezi minne ilipita akampigia simu mama yake na kumwambia yupo Dubai anafanya kazi, tulipochunguza namba ilionesha yupo China, tukaambiwa huwa hawatakiwi kusema ukweli wa sehemu walipo.”
BIASHARA ILIVYO
Uchunguzi unaonesha kuwa, mawakala wanaosafirisha wasichana wa Kibongo kwenda China, Dubai au India, wakifika, huwanyang’anya hati zao za kusafiria ili washindwe kuondoka nchini humo na kushinikizwa kujiuza (ukahaba) huku wao mawakala wakipokea fedha kutoka kwa wateja.
Uchunguzi unaonesha wasichana hao hurejeshewa hati zao baada ya malipo ya kiasi cha Dola za Marekani 8,000 (kama shilingi milioni 12).
Marehemu Habiba Yusuph Ally (kushoto) wakati akiwa shule.
Wengi wakishaachiwa hushindwa kurejea Bongo na kujikuta wakiendelea kuuza miili katika mahoteli na klabu huku wakikutana na majanga mbalimbali.

BBC YAZINDUA STUDIO ZAKE NCHINI, KIPINDI CHA ASUBUHI CHA AMKA NA BBC KURUKA MOJA KWA MOJA KUTOKEA DAR

Mkuu wa Habari wa BBC Idhaa ya Ulimwengu,Bi. Nikki Clarke akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kituo cha kurushia Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC jijini Dar es Salaam,katika Jengo lao lililopo Mikocheni.Kushoto ni Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Ali Saleh (wa tatu kulia) akiwapatia maelekezo Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Dkt. Salim Ahmed Salim na Mwenyekiti wa CUF,Prof. Ibrahim Lipumba namna ya Idhaa hiyo inavyoandaa vipindi vyake na inavyopeleka hewani wakati wa hafla ya Uzinduzi rasmi wa Kituo cha kurushia Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC,jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC jijini Dar es Salaam,Hassan Mhelela (kushoto) akizungumza katika hafla hiyo pamoja na kuitambulisha timu yake.
Taswira ya Studio za BBC jijini Dar.
Chumba cha Habari cha BBC jijini Dar.Picha zote na Othman Michuzi.

Saturday, July 19, 2014

SPIKA ANNE MAKINDA AWASILI ARUSHA, AKAGUA UKUMBI UTAOTUMIKA KATIKA MKUTANO WA 45 WA MABUNGE WA NCHI WANACHAMA WA JUMUIYA YA MADOLA

Spika wa Bunge, Mhe Anne Makinda akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe Magese Mulongo (kulia) baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Arusha, jana tayari kwa  kuhudhuria Mkutano wa  45 wa Mabunge wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kwa Kanda ya Bara la Afrika utakaoanza tarehe 20 hadi 27 Julai Mjini Arusha .
Spika wa Bunge, Mhe Anne Makinda akipewa maelezo na Mkurugenzi wa Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa Jossey Mwakasyuka alipokwenda kukaguwa Ukumbi wa Ngurudoto, Arusha , jana, patakapofanyika Mkutano wa  45 wa Mabunge wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kwa Kanda ya Bara la Afrika ambapo Tanzania ni mwenyeji wa kongamano hilo.
Spika wa Bunge, Mhe Anne Makinda akitowa maelekezo kwa kamati ya maandalizi ya Mkutano wa  45 wa Mabunge wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kwa Kanda ya Bara la Afrika alipotembelea Ukumbi wa Ngurudoto, mkoani Arusha  patakapofanyika kongamano hilo ambapo Tanzania ndio mwenyeji

TAMASHA LA USIKU WA MATUMAINI 2014 ' NDONDI ZA MWAKA'



Jaja aanza kazi Yanga, afanya balaa mazoezini

Straika mpya Yanga, Mbrazili, Genilson Santana Santos ‘Jaja’,
Na Sweetbert Lukonge
STRAIKA mpya Yanga, Mbrazili, Genilson Santana Santos ‘Jaja’, tayari ameanza kuonyesha makeke yake baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu katika mazoezi ya timu hiyo yaliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Sokondari Loyola, Mabibo, jijini Dar es Salaam, jana.
Jaja, tangu atue hapa nchini Jumanne iliyopita akitokea Brazil, alikuwa hajawahi kufanya mazoezi ya kucheza mpira, siku zote alikuwa akifanya mazoezi ya kukimbia ili kujiweka fiti tayari kwa kuungana na wachezaji wenzake wanaoendelea na programu za kocha wa timu hiyo, Marcio Maximo kwa ajili ya michuano ya ligi kuu msimu ujao na ile ya kimataifa.
Hata hivyo, katika mazoezi ya jana ambayo Jaja alijumuika na wachezaji wenzake katika kuuchezea mpira ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ajiunge na timu hiyo, alionyesha uwezo mkubwa wa kuzifumania nyavu.
Katika mazoezi hayo ambayo wachezaji wa timu hiyo walikuwa wakifundishwa na Maximo jinsi ya kufunga pindi wanapokuwa katika eneo la hatari, Jaja alipiga mashuti nane na matano kati ya hayo yalitinga wavuni.
Mashuti matatu alimfunga Juma Kaseja na mawili alimfunga Ally Mustapha ‘Barthez’, jambo ambalo liliwafanya mashabiki wengi waliokuwa wakiangalia mazoezi hayo kumpigia makofi mchezaji huyo.
Mchezaji mwingine aliyefanya vizuri katika mazoezi hayo alikuwa ni Hamis Thabiti ambaye alizifumania nyavu mara sita na kukosa mashuti miwili.

Azam, Mtibwa kunogesha Tamasha la Matumaini

Kikosi cha timu ya Azam, FC
Na Khadija Mngwai
TIMU za Azam FC na Mtibwa Sugar, zinatarajiwa kunogesha Tamasha la Usiku wa Matumaini litakalofanyika Agosti 8, mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa kushuka dimbani siku hiyo kuonyeshana ubabe.
Tamasha hilo litahusishwa na burudani kibao ikiwa ni pamoja na mechi za Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande wa Simba na Yanga ambao wataonyeshana ubabe kwa kujua nani mkali.
Kikosi cha timu ya Mtibwa Sugar,
Mwaka jana, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, alipuliza kipenga kuashiria mtanange huo kuanza kati ya wabunge ambapo safari hii wataonyeshana uwezo wa hali ya juu kufuatia kila upande kutaka kuibuka na ushindi.
Mechi hiyo ya Azam na Mtibwa itaanza mapema kabla ya mechi ya waheshimiwa. Mtanange wa timu hizo za ligi kuu, utachezwa kwa dakika 90 na kutoa fursa kwa timu hizo mbili kuonyesha vikosi vyao vipya kwa ajili ya msimu ujao.