Na Sweetbert Lukonge
STRAIKA
mpya Yanga, Mbrazili, Genilson Santana Santos ‘Jaja’, tayari ameanza
kuonyesha makeke yake baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wa kuzifumania
nyavu katika mazoezi ya timu hiyo yaliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya
Sokondari Loyola, Mabibo, jijini Dar es Salaam, jana.
Jaja, tangu atue hapa nchini Jumanne iliyopita akitokea Brazil,
alikuwa hajawahi kufanya mazoezi ya kucheza mpira, siku zote alikuwa
akifanya mazoezi ya kukimbia ili kujiweka fiti tayari kwa kuungana na
wachezaji wenzake wanaoendelea na programu za kocha wa timu hiyo, Marcio
Maximo kwa ajili ya michuano ya ligi kuu msimu ujao na ile ya
kimataifa.
Hata hivyo, katika mazoezi ya jana ambayo Jaja alijumuika na
wachezaji wenzake katika kuuchezea mpira ikiwa ni mara yake ya kwanza
tangu ajiunge na timu hiyo, alionyesha uwezo mkubwa wa kuzifumania
nyavu.
Katika mazoezi hayo ambayo wachezaji wa timu hiyo walikuwa
wakifundishwa na Maximo jinsi ya kufunga pindi wanapokuwa katika eneo la
hatari, Jaja alipiga mashuti nane na matano kati ya hayo yalitinga
wavuni.
Mashuti matatu alimfunga Juma Kaseja na mawili alimfunga Ally
Mustapha ‘Barthez’, jambo ambalo liliwafanya mashabiki wengi waliokuwa
wakiangalia mazoezi hayo kumpigia makofi mchezaji huyo.
Mchezaji
mwingine aliyefanya vizuri katika mazoezi hayo alikuwa ni Hamis Thabiti
ambaye alizifumania nyavu mara sita na kukosa mashuti miwili.
No comments:
Post a Comment