Wakati vikao vya Bunge Maalum la Katiba vikiendelea tena mjini Dodoma
wiki hii bila ya kuwepo kwa kikundi kinachojiita Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samweli Sitta amesema
amekuwa akisisitiza kuwa bunge hilo halitaahirisha shughuli zake hadi
hapo muda wa siku 60 waliopewa utakapokamilika.
Sitta alisema rasimu hiyo ina mambo mengi mazuri lakini pia akasema
kuna mambo mengine yanatakiwa kufanyiwa marekebisho ili Watanzania
waweze kupata katiba bora.
Ni kweli kwamba maudhui ya rasimu ya katiba yanajumuisha baadhi ya
mambo yafuatayo; kuimarisha Muungano wetu kwa kuleta uwiano bora wa
mamlaka ya Zanzibar na Tanzania Bara ndani ya Muungano, kuimarisha haki
za binadamu na kuzuia wachache kufuja rasilimali za taifa.
Naamini upo ukweli kwamba ndani ya rasimu hiyo inayojadiliwa yapo
mapungufu kwa kuachwa masuala ya kuwezeshwa kuundwa kwa Serikali za
Mitaa, maelekezo ya matumizi ya ardhi na rasilimali nyingine.
Hakika
kitendo kinachofanywa na wajumbe wa bunge hilo wanaounda Ukawa ni
kibaya kwani kususia kikao si jambo jema na badala yake wangelumbana kwa
hoja ndani ya bunge.
Niwaombe tu wana Ukawa kwamba waache kupotosha umma na kuonekana kuwa
wao ni bora zaidi ya wajumbe wengine walioko ndani ya Bunge Maalum la
Katiba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Pandu Amir Kificho tayari
amewasilisha mapendekezo ya kanuni 12 ambazo zitaliwezesha bunge hilo
kukamilisha kazi yake katika muda uliopangwa wa siku 60.
Mapendekezo hayo yalipitishwa katika moja ya kikao cha jioni wiki
iliyopita kwa kauli moja kutoka kwa wajumbe waliokuwepo na hivyo kazi ya
kuanza kujadili sura zilizobaki zikaanza na zitaendelea wiki hii.
Kwa kumbukumbu zangu ni kwamba awali akichangia mapendekezo hayo,
mjumbe wa bunge hilo na Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangala alisema
kuundwe kanuni itakayowabana wajumbe waliotoka katika Bunge hilo na hata
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji
Joseph Sinde Warioba iliyoshughulikia mchakato wa ukusanyaji maoni
kutoingilia mwenendo wa bunge hilo wakati huu vikao vyake vinapoendelea.
Ni jukumu la wapenda amani wote katika nchi hii kuwahimiza Ukawa
kuingia katika meza ya maridhiano kwa sababu muda bado upo na ni vizuri
sana wakaingia sasa bungeni kwa sababu yanayojadiliwa yanawagusa
wananchi katika majimbo yao moja kwa moja.
Nizidi kumuomba Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe kuliona hili na
kukumbuka wahenga waliosema kuwa hakuna vita inayokwisha nje ya meza ya
mazungumzo. Hii ni hoja yangu, muitafakari tafadhali. Wanachi wote
wanataka Katiba mpya itakayodumu miaka 50 ijayo.
No comments:
Post a Comment