Thursday, March 13, 2014

TAARIFA KWA UMMA: VIPINDI VYA MVUA KUBWA VINATARAJIWA

SAMIA HASSAN NDIYE MAKAMU MWENYEKITI BUNGE LA KATIBA


Samia Suluhu Hassan.
Samia Suluhu Hassan ndiye Makamu Mwenyekiti wa Kudumu Bunge Maalum la Katiba baada ya kupata kura 390 sawa na 74% na kumshinda mpinzani wake Amina Abdallah Amour aliyepata jumla ya kura 126 sawa na 24%. Kwa matokeo hayo, Samia Hassan ataungana na Samuel Sitta aliyechaguliwa jana kuwa Mwenyekiti wa Kudumu wa bunge hilo katika mchakato mzima wa kupata katiba mpya.`

RAHA YAPANUA WIGO WA MAWASILIANO YA INTERNET TANZANIA


Mkurugenzi Mkuu wa Biashara wa Raha, Akash Karia (kushoto) akielezea huduma za internet zitolewazo na Raha kwa wanahabari (hawapo pichani). Pembeni ni viongozi wa kampuni hiyo.
Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakimsikiliza Akash.
Mkurugenzi Mkuu wa Teknolojia, Nyangu Meghji (katikati) akielezea maboresho yaliyofanywa na Raha katika huduma za internet.Viongozi wa Raha wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mkutano na wanahabari.
KAMPUNI inayotoa huduma za internet nchini, Raha, imepanua wigo wa mawasiliano katika internet kwa kutumia teknolojia za 4G WiMax Solution pamoja na Fiber Optic.
Raha kwa sasa wanatoa huduma za internet katika mikoa mbalimbali nje ya Dar es Salaam ikiwemo Tanga na Arusha kwa kutumia teknolojia ya rahaSpots ambayo inamuwezesha mteja kupata huduma bora popote alipo.
Kwa maboresho haya, Raha wanawaahidi huduma bora zaidi wateja wake ikiwemo kuperuzi kwa haraka mitandao mbalimbali ya kijamii na tovuti.

RAIS WA BAYERN MUNICH AHUKUMIWA KWENDA JELA MIAKA 3 KWA KUKWEPA KODI


Rais wa Bayern Munich, Uli Hoeness.
Rais wa Bayern Munich amehukumiwa kwenda jela kwa kifungo cha miaka mitatu na miezi sita kutokana na kosa la kukwepa kodi.
Uli Hoeness, 62, alikiri kukwepa kodi inayofikia kiasi cha €18.5 million kupitia akaunti zake za benki za siri lakini utetezi wake wa kukiri kosa akidhania ungemsaidia kuepukana na adhabu ya kifungo ulishindwa kumsaidia.
Mwendesha mashtaka alitaka Hoeness afungwe jela miaka mitano na nusu kwa kutokana na kupatikana na hatia ya kukwepa kodi.
Mwishowe, jaji wa mahakama iliyokuwa ikisikiliza kesi hiyo akaamuru mwanasoka huyo wa zamani wa Ujerumani Magharibi atumikie kifungo cha miaka 3 na miezi sita.

GARI LA WIZARA ZANZIBAR LAPINDULIWA KWA MAWE!



Habari zilizopatikana mchana huu kutoka visiwani Zanzibar zinasema kuwa vijana wenye mikokoteni inayovutwa na Ng'ombe wamefanya vurugu na kuanza kupiga mawe magari ya serikali huku wakijerui wafanyakazi wa serikali kadhaa. Katika kadhia hiyo, walisababisha gari la Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Uchumi,  Mhe. Khamis Musa kupinduka kama linavyoonekana pichani. Inaelezwa kuwa chanzo cha vurugu hizo ni kupigwa marufuku kwa mikokoteni hiyo kuingia mjini, kitendo ambacho kinapingwa na wamiliki.

RAIS KIKWETE APOKEA RIPOTI YA MGAWANYIKO WA WATU KWA UMRI NA JINSI LEO IKULU, DAR


Rais Jakaya Mrisho Kikwete akipokea toka kwa   Kamishna wa Sensa Hajjat Amina Mrisho Ripoti ya Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia kwa data za sensa ya watu na makazi mwaka 2012 leo Machi 13, 2014   Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Kamishna wa Sensa Hajjat Amina Mrisho (kushoto) na  Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa  baada ya kupokea Ripoti ya Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia kwa data za sensa ya watu na makazi mwaka 2012 leo Machi 13, 2014  Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa ambaye pamoja na Kamishna wa Sensa Hajjat Amina Mrisho baada ya kupokea Ripoti ya Mgawanyo wa Watu kwa Umri na Jinsia kwa data za sensa ya watu na makazi mwaka 2012 leo Machi 13, 2014   Ikulu jijini Dar es Salaam.

USIJIDANGANYE, NDOA SIYO MAJARIBIO!-2


NDOA ni kitu chenye thamani kubwa sana katika maisha ya binadamu. Jambo na la msingi zaidi kwa wahusika ambao wanahitaji kuunganika katika ndoa ni upendo.
Lazima wote wawe wana hisia za kweli kutoka ndani ya mioyo yao.
Ndoa si jambo la kukurupuka wala kuamua kuingia kwa maana ya kufanya majaribio. Siyo sahihi hata kidogo.
Wiki iliyopita nilianza kwa kueleza mambo ya msingi ya kuzingatia wakati ukimtaka mwenzi wa maisha yako. Leo tunaingia katika hatua nyingine. Twende tukaone.
MAPENZI HALISI
Sifa nyingine muhimu ya kumwangalia mwenzi anayefaa kuwa naye kwenye ndoa ni pamoja na yule mwenye mapenzi ya kweli hasa. Mapenzi ya kweli huonekana haraka sana. Penzi la dhati halijifichi.
Hujitokeza hadharani, wakati mwingine bila hiyari.
Mwenye sifa hii ni msikivu (kwa wanaume na wanawake), muelewa na anayetoa kipaumbele kwa mwenzake. Kama anakupenda kwa dhati ni lazima akupe kipaumbele katika mambo yake.
Si msiri na hutoa nafasi kwa mwenzake kutoa mawazo yake katika mambo yanayomhusu. Hatua hii hutokana na namna anavyomuona mwenzake kama sehemu ya maisha yake.
HUYU HAFAI!
Unaweza kuwa na mpenzi na mkapanga mipango mbalimbali ya baadaye ikiwemo ndoa lakini akawa na kasoro kubwa zilizojificha. Wakati mwingine kasoro hizo unaweza kuziona lakini usijue kama ni kubwa zinazoweza kuwa tatizo kubwa katika maisha yenu ya ndoa.
Mara nyingi kasoro za mwingine zinaweza kufichwa na mapenzi ya dhati yaliyopo ndani ya mtendwa. Mathalani wewe una mpenzi wako, kwa vile ndani yako kuna mapenzi ya dhati, mwenzako anaweza kuwa anakosea tena makosa makubwa, lakini ukajikuta unavumilia, kudharau au kupuuzia!
Zipo dalili nyingi za mpenzi asiyefaa, lakini hapa nakuletea zile za muhimu zaidi.
USALITI
Katika makosa makubwa kabisa kwenye uhusiano ni pamoja na kusaliti. Kama mwenzi wako anakusaliti na una ushahidi wa kutosha (hasa kama umemfumania) ni dalili mbaya kwenye ndoa.
Mtu wa aina hiyo hafai kabisa kumfikiria kuungana naye katika ndoa.
KIBURI
Pia ni dalili mbaya. Mtu mwenye dharau na kiburi hawezi kuwa sahihi, maana huko ndani ya nyumba kutakuwa ni majibizano yasiyo na maana.
Aliye sahihi anapaswa kuwa msikivu, mwenye kupima kila kinachotoka kwenye ulimi wake. Kama katika kipindi cha awali tu, anakuwa mkorofi, vipi kwenye ndoa? Fikiri hili kwa makini.

KIPIGO
Wengi wanaweza wasione kama hili lina maana, lakini nataka kuwaambia, mtu anayetumia nguvu na kumwadhibu mwenzake kwa kipigo, siyo mwenzi sahihi.
Tabia hii zaidi ipo kwa wanaume. Kosa dogo tu anamwangushia mwenzake kipigo. Kupigana si mapenzi. Kama bado mpo kwenye uchumba tu, kosa dogo kipigo, vipi mkiingia kwenye ndoa? Tafakari jambo hili utaona ni kasoro kubwa sana.

MBINAFSI
Hili ni tatizo lingine. Kama mnahitaji kuwa katika muunganiko wa ndoa, ubinafsi ni sumu. Mwenzi mwenye tabia ya lake linakuwa lake mwenyewe na lako linakuwa lenu hafai kwenye ndoa.

ASIYEJITOA
Hili nalo ni tatizo. Unaweza kuwa na tatizo kubwa na kwa kulitazama unaamini kabisa kwamba mwenzako anaweza kukusaidia, lakini hataki tu. Mathalani unaumwa, anaweza kushindwa hata kufika kukujulia hali - hafai.
Hata kama unampenda kwa kiwango gani, huyu hafai kabisa kuwa nawe kwenye ndoa.
Wiki ijayo tunaingia katika sehemu ya mwisho ya mada hii, USIKOSE!

UFUSKA LOKESHENI


STORI: ERICK EVARIST
BAADHI ya wasanii wa filamu za Kibongo hivi karibuni walinaswa wakifanya vitendo vichafu katika eneo lao la kurekodia ‘location’ pande za Oysterbay jijini Dar, Ijumaa lina uthibitisho wa kutosha.
Wasanii wa filamu wakipozi kwa picha tata.
Kwa mujibu wa chanzo chetu wasanii hao walinaswa wakifanya vitendo hivyo vilivyo nje ya maadili ya Mtanzania kwa uwazi bila ya kumuogopa mtu yeyote.
Chanzo chetu kilijipenyeza katika kambi ya wasanii hao iliyopo eneo hilo na kuwanasa wakifanya vitendo hivyo vichafu.
...Pozi lingine la kichokozi la wasanii hao waliokuwa lokesheni.
“Wameweka kambi kwenye nyumba moja Mikocheni na wamekuwa wakienda kushuti kwenye Ufukwe wa Coco, yaani nimekuwa nikiwafuatilia matendo yao, siyo mazuri. Wanavaa nguo nusu utupu, wanafanya vitendo vinavyoashiria usagaji mbele za watu bila aibu, njooni muwafichue.
“Kuna picha ambazo nimewapiga bila wao kujijua, zinatia kinyaa, mbaya zaidi wengi wao ni wadogowadogo na huenda wamewadanganya wazazi wao kuwa wameenda shule kumbe wapo huku,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya paparazi wetu kushibishwa madai hayo na kuziona picha hizo chafu,  aliwafuatilia wasanii hao na kuwatambua kwa majina  waliohusika kufanya uchafu huo kuwa ni Leticia, Ania pamoja na  mchekeshaji wa siku nyingi, Jabir Ally ‘Wajajo’.
Alipotafutwa Wajajo kuzungumzia picha hizo alisema: “Sidhani kama ni makosa watu kujiachia ufukweni, labda kwa waliofanya vitendo vya kisagaji ndiyo watakuwa wamekosea…tulikuwa lokesheni tukirekodi filamu tukawa tumejiachia, inawezekana wengine walipitiliza.”

Nyota 9 wayeyuka mazoezini Simba

Mshambuliaji wa simba,Betram Mwombeki.
Na Martha Mboma
WACHEZAJI tisa wa Simba walishindwa kufika mazoezini kwenye Uwanja wa Kinesi, Shekilango jijini Dar, jana kutokana na sababu tofauti ikiwemo ya majeraha na matatizo ya kifamilia.
Donald Musoti.
Wachezaji hao ni Amissi Tambwe ambaye ana jeraha kichwani, Zahoro Pazzi ambaye ana tatizo la enka na Gilbert Kaze anayesumbuliwa na goti.
Wengine ambao ni majeruhi ni: Donald Musoti, Betram Mwombeki, Said Ndemla, Abubakari Hashimu, Uhuru Selemani na Abdulhalim Humud ambapo wote hawa wawili wana matatizo ya kifamilia.
Uhuru Selemani.
Kocha Mkuu wa Simba, Zdravok Logarusic, amesema asilimia kubwa ya kikosi chake ni majeruhi ndiyo maana hawaonekani mazoezini hapo kwa siku kadhaa.
“Ninaamini wachezaji wote hao tutakuwa nao pamoja tutakapoanza mazoezi Jumatatu,” alisema Loga.