Na Wilbert Molandi
KOCHA Mkuu wa
Yanga, Mbrazili, Marcio Maximo, amepanga kuthibitisha kuwa yeye ni bora
kwa kutumia mifumo minne katika mechi za Ligi Kuu Bara na Kombe la
Shirikisho Afrika.
Kauli hiyo ameitoa kocha huyo akiwa na wiki tatu
tangu aanze kukinoa kikosi hicho kinachojiandaa na ligi na michuano ya
kimataifa watakayoshiriki mwakani.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Maximo alisema katika mifumo hiyo
atakayoitumia, itategemea na aina ya timu atakayocheza nayo ndani ya
uwanja.
Maximo alisema wakati mechi inaendelea, anaweza kubadili mfumo baada ya kuona ule anaoutumia haumpi matokeo mazuri ya ushindi.
Mbrazili huyo aliitaja mifumo atakayoitumia katika mechi zake kuwa ni
4-4-2, 4-3-3, 4-5-1 na 4-3-2-1 ambayo kati ya hiyo itategemeana na timu
anayocheza nayo.
“Ni ngumu kutaja mfumo mmoja ninaoutumia katika mechi zangu, kikubwa
unachotakiwa kufahamu ni kuwa, mimi nina mifumo ya aina nne na yote
huenda nikaitumia katika mechi moja.
“Hiyo inategemeana na aina ya
timu ninayocheza nayo, mechi nyingine ni ngumu ambazo zinahitaji kulinda
goli lenu na nyingine inayohitaji viungo wengi, hivyo unahitaji
kubadili mfumo haraka.
“Mifumo yote hiyo ninawafundisha wachezaji wangu katika mazoezi,
lengo ni kuishika na kuitumia wakiwa ndani ya uwanja,” alisema Maximo.
Aidha, kocha huyo anaendelea kukiimarisha kikosi chake ambapo tangu
atue kuifundisha Yanga, anaiboresha safu ya ushambuliaji kwa kuwapa
mbinu mbalimbali za ufungaji mabao washambuliaji wake.
“Tatizo la ushambuliaji ni kubwa nchini, ndiyo maana tangu nimeanza
kuifundisha Yanga, ninawapa washambuliaji wangu mbinu za ufungaji.”
Katika hatua nyingine, Maximo amemtema kiungo mshambuliaji, Reliants Lusajo na beki wa pembeni, Abuu Ubwa kwenye kikosi chake.
Maximo aliwarejesha wachezaji hao ili aangalie viwango vyao baada ya
hivi karibuni uongozi wa timu hiyo kutangaza kuwatema pamoja na mwezao
Hamis Thabiti aliyebakizwa.
Maximo alisema kuwa amewaondoa nyota hao
rasmi katika kikosi chake atakachokitumia kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu
Bara na Kombe la Shirikisho Afrika.
Maximo alisema, amefikia hatua ya kuwatema wachezaji hao kutokana na kutoridhishwa na viwango vyao katika mazoezi.
Aliongeza kuwa, amemrejesha kiungo Thabiti katika kikosi chake
kutokana na kuridhishwa na kiwango chake alichokionyesha kwa muda wa
wiki mbili alizompa.
“Ujue nilivyoondoka nchini na kurudi nyumbani
kwetu Brazil, niliondoka na faili la wachezaji niliokuwa nawafundisha,
kati ya hao alikuwepo Ubwa na Thabiti wakiwa na umri mdogo wanaichezea
timu ya taifa ya U20.
“Hivyo nilivyorudi niliwaulizia wachezaji nikaambiwa walisajiliwa na
Yanga na kutemwa kabla ya kuwaita kwenye mazoezi yangu kuona viwango
vyao kabla ya kuwarejesha, pia nikatajiwa Lusajo kuwa ana umri mdogo
ambaye nilimuita naye.”
Wakati huo huo, Maximo amekuja na mpya katika timu hiyo kwa kutaka kila mchezaji kucheza nafasi zaidi ya moja ndani ya uwanja.
Maximo alisema, hataki kikosini kwake amtegemee mchezaji mmoja, hivyo
amepanga kuwafundisha wachezaji wake katika mazoezi ili wacheze namba
tofauti.
“Ukifuatilia katika mazoezi yangu, utaona ninawafundisha wacheze nafasi zaidi ya moja ndani ya uwanja kwenye mechi zetu.
“Mchezaji kama Twite (Mbuyu) nimemkuta anacheza namba mbili, lakini
tangu nimekuja ninamtumia katika mazoezi yangu kucheza kiungo mkabaji,
namba mbili na tatu.
“Pia Javu (Hussein), Bahanuzi (Said) na wengine wengi wakiwemo
wachezaji wa U20 niliowapandisha katika kikosi cha wakubwa nahakikisha
wanacheza nafasi nyingi ili siku ikitokea mmoja akapata majeraha au
kadi, basi nitatumia mchezaji mwingine kuchukua nafasi yake,” alisema
Maximo.
No comments:
Post a Comment