Saturday, July 19, 2014

MASWALI 10 YA KUJIULIZA KABLA YA KUACHANA(TALAKA)-4

Mapenzi ni wewe mwenyewe unavyojiweka. Kuna makosa mengi yamekuwa yakitokea katika kuachana na kusababisha majuto ya baadaye. Makala haya lengo lake ni kukutaka kabla ya kuachana, ni vizuri kujiuliza maswali ambayo ama yatakufanya ujirudi na kuujenga upya uhusiano wako au kuachana ukiwa na hoja za msingi.
Kwa kuendelea tulipoishia wiki iliyopita ni kuwa elimu sahihi ya utatuzi wa migogoro ya kimapenzi na uhusiano inatoa muongozo kuwa kwenye kila hali ya kuhitilafiana na baadaye kuachana, lazima pande zote mbili ziwe zimechangia. Kwa maana hiyo, usikimbilie kusema “mwenzangu ni tatizo’, jiulize “nimechangia nini kwenye huu mgogoro?”
Grisi hufanya chuma kuwa laini, swali hilo nalo ni grisi inayoweza kuulaini moyo wako na fikra zako kisha kukufanya kujirudi na kuutetea uhusiano wako usiende na maji. Tafiti zinaonesha kuwa bila kuangalia aina ya makosa ambayo wapenzi wametendeana, asilimia 90 ya waliojirudi na kila mmoja kujisahihisha, walivuka wakiwa imara.
Ushauri kwako ni kwamba jaribu kujishusha kwenye mgogoro wako na mwenzi wako. Usiangalie nani katenda, kwani muhimu kwako ni penzi lako kuwa endelevu. Ukiona wewe huwezi kujishusha basi hiyo itakujengea tabia ya kujiona bora sana, hata mbele ya safari utakutana na mwingine na mambo yatakuwa yaleyale. Jitazame, jikosoea!
SAPOTI YAKO KWA MPENZI WAKO IPOJE?
Usisahau kujiuliza swali hili! Inawezekana mwenzi wako mnatofautiana kwa sababu humuoneshi sapoti yoyote. Haya maisha yana changamoto nyingi sana, hakuna kitu kizuri kama pale mwenzio anapokuona upo naye bega kwa bega katika kuzikabili na kuzishinda mkiwa pamoja.
Hakuna jambo linaloumiza kama pale ambapo mwenzi wako anakutana na vipindi vigumu lakini kila anapotafuta uwepo wako inakuwa shida. Hakuoni na kumfanya ajihisi yupo peke yake. Wakati wa kuelekea kuachana na mwenzio, unapojiangalia na kugundua hujampa sapoti, jirekebishe.
Maisha yamejaa mapambano, hata kama umetulia peke yako, unaweza kujikuta upo kwenye pambano lisilo rasmi na mtu. Kwa kifupi ni kuwa migongano na watu kwenye maisha hayakwepeki. Sasa wewe nafasi yako ipoje pale mpenzi wako anapokuwa kwenye matatizo?
Si ajabu wewe ukawa karibu na mtu ambaye ana uhasama na mwenzi wako. Jiulize hapo unakuwa unamsaidia mwenzi wako au unamuumiza? Hakuna kosa kubwa ambalo unaweza kulifanya kama la kukubali kuachana na mwenzi wako bila kufanya tathmini ya mchango wako kwake. Je, ni chanya au hasi?
Jiulize hata wewe mwenyewe, ghafla tu umejikuta unagombana na mtu, ukiwa unatarajia kuwa mpenzi wako atakuwa nawe bega kwa bega, inakuwa tofauti kabisa. Mpenzi wako yupo mbali na hata hajishughulishi angalau kukutia moyo au kukupa ushauri unaoweza kukufanya ujione haupo peke yako.
Si hivyo tu, unajikuta mwenzi wako anakuwa karibu na mtu ambaye anakupiga vita.
Kwa hayo mawili, mwenzio kuwa mbali nawe au kuwa karibu na adui, unajisikiaje? Jawabu hilo likuongoze kutambua kuwa naye anapokukosa nyakati ambazo anahitaji kampani yako, ni maumivu makubwa kwake.
Sapoti haipo kwenye mapambano tu, inahusu harakati mbalimbali. Anapokuwa kwenye uhitaji mkubwa, nafasi yako ipoje? Anapokuwa anaumwa, wewe unakuwa wapi? Kuna jambo analitaka sana na endapo atalifanikisha furaha yake itakuwa imekamilika, je, unamsadiaje kufikia hayo malengo?
Kabla hujaachana naye, hakikisha umeangalia maeneo yote na kugundua kwamba sapoti unayompa ni kubwa lakini yeye ameshindikana. Jitahidi kujisahihisha pale unapogundua kuwa hukuwa ukimpa sapoti ya kutosha. Pengine hiyo inaweza kuwa chanzo cha mgogoro, kwa hiyo ukijirudi unaweza kufanya uhusiano wenu uwe imara sana.

No comments:

Post a Comment