WAZIRI MKUU APIGIA KURA VIVUTIO VYA TANZANIA
Waziri Mkuu Mh. Mizengo Peter akipata maelekezo ya namna ya
kupiga kura yake kutoka kwa Meneja wa Tawi la Bodi ya Utalii Tanzania(TTB)
Arusha Bw. Wily Lyimo muda mfupi kabla ya kupiga kura yake katika kituo cha
Mikutano cha AICC mjini Arusha hivi karibuni.
Na Geofrey Tengeneza
Waziri Mkuu Mheshimiwa Mizengo Pinda hivi karibuni amepiga kura yake ya kuvichagua
vivutio vitatu vya Tanzana katika shindano linaloendelea hivi sasa la kutafuta
maajabu Saba ya asili ya Afrika.
Waziri Mkuu alipiga kura yake wakati wa mkutano wa tano wa
wadau wa Mfuko wa Pensheni wa LAPF uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa
mikutano wa AICC mjini Arusha ambapo Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iliweka
kituo cha kupigia kura kwa njia ya mtandao wa komputa (internet).
Waziri Mkuu alivipigia kura vivutio hivyo vitatu ambavyo ni
Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Kreta ya Ngorongoro ili
viweze kuwa miongoni mwa maajabu Saba ya Asili
barani Afrika.
Viongozi wengine
waliopiga kura zao wakati wa mkutano huo katika kituo hicho cha Bodi ya utalii
Tanzania ni pamoja na Waziri wa Kazi na Ajira
Mh.Gaudensia Kabaka, Naibu Waziri wa TAMISEMI Mh.Henry Mwanri na
viongozi mbalimbali wa LAPF.
Bodi ya Utalii Tanzania hivi sasa inaendesha
kampeni kamambe ya kuwahamasisha watanzania kuvipigia kura vivutio hivyo, na
katika mkutano huo iliamua kupiga kambi katika kituo hicho cha mikutano ya
Kimataifa cha AICC kwa lengo la kuwahamashishawajumbe wa mkutano huo na
kuhakikisha wale ambao hawajapiga kura wanapiga kura zao katika kituo hicho
hapo AICC zoezi ambalo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
No comments:
Post a Comment