Stori: Imelda Mtema na Ojuku Abraham YULE
‘hendsam’boi’ Michael Christian (28) ambaye mwaka jana aliitikisa
medani ya siasa Bongo kufuatia kufunga ndoa na Mbunge wa Viti Maalum
(CCM) Mkoa wa Rukwa, Rose-Sweeter Kasikila (60) na miezi michache mbele
ndoa ikavunjika, ameibuka na kuanika siri 7 zilizomfanya aamue kuivunja
ndoa hiyo na mheshimiwa huyo.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Mkoa wa Rukwa, Rose-Sweeter Kasikila.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar, juzi, Michael alibainisha mambo hayo huku akisema anajuta kwa tukio lile ambalo bado halijamtoka kichwani hadi sasa.
Michael Christian‘hendsam’boi’ aliyevunja ndoa na ndoa hiyo na mheshimiwa huyo ndani ya Ofisi za Global.
SIRI YA KWANZA Kijana Michael aliianika siri ya
kwanza kwamba ni kuchekwa na marafiki zake wa Bagamoyo mara baada ya
kugundua amefunga ndoa na mbunge huyo ‘mzee’.
“Marafiki zangu
walianza kunicheka, walisema nimefunga ndoa na mbunge mzee, mama mtu
mzima. Nikaanza kujisikia vibaya jambo ambalo sikulipenda hata kidogo,”
alisema kijana huyo ambaye ni yatima.
SIRI YA PILI
Akizungumza kwa hisia kali, Michael aliye na taaluma ya uuguzi,
aliiweka wazi siri ya pili ya kuamua kuivunja ndoa yake na mheshimiwa
huyo kuwa ni kitendo cha kutokuwepo kwa tangazo la ndoa la siku 21 kama
sheria ya nchi inavyotaka.
Kuna kifungu cha sheria kinachotaka
wachumba wanapotaka kufunga ndoa kutolewa tangazo la siku 21 kwenye
mamlaka za kufungisha ndoa hiyo ili kama mmoja wa wahusika ana ndoa
inayoishi (halali) aweze kuwekewa pingamizi la kufungishwa ndoa.
SIRI YA TATU
Kijana huyo aliendelea kwa kuifunua siri ya tatu kuwa ni kitendo cha
kufungishwa ndoa bila kuwepo na mashahidi wa pande zote mbili (matroni
na patroni) walioandaliwa zaidi ya kuitwa papohapo.
Alimtaja kwa
jina moja Mchungaji Mtetumo wa Kanisa la Mikocheni ‘B’ Assemblies of God
‘Mlima wa Moto’ kuwa ndiye aliyesimamia kufungwa kwa ndoa hiyo,
Septemba Mosi, 2011 ndani ya ofisi huku milango ikiwa imefungwa.
Alisema pia kwamba, suala la ndoa aliligundua siku hiyohiyo baada ya
kufika kwenye kanisa hilo ambapo maandalizi mengine yote yalishafanyika
akiwa hajui.
SIRI YA NNE Siri zilizidi
kubanjuliwa, Michael alisema sababu ya nne ambayo pia ilimsukuma kuamua
kubatilisha ndoa yake na mama Kasikila ni baada ya kubaini kwamba,
hataweza kupata uzao kwa mke huyo kwa sababu ana watoto wakubwa kiumri
kuliko yeye.
“Nilijua sitapata watoto, hakukubali kuzaa na mimi kwa
sababu tayari ana watoto wakubwa, mimi mdogo, ingekuwa vigumu. Kifupi
haikuwa ndoa halali kwangu,” alisema kijana huyo.
SIRI YA TANO
Michael: “Alianza kunibana sana, kila hatua ya miguu yangu alitaka
kujua inakwenda mpaka wapi! Hii hali nikaiona inanipiga pingu,
nikagundua kuwa kumbe mimi sijaoa, bali nimeolewa. Yule mama alinioa
mimi, si kwamba mimi nilimuoa yeye, nikasema ili niwe na amani ya moyo
ni lazima ndoa ivunjike.”
SIRI YA SITA Kijana huyo hakuona sababu ya kubakiza siri hata moja, akaendelea kuzianika:
“Jambo jingine ambalo pia lilichangia kuamua kuivunja ndoa ile ni baada ya kukumbuka historia ya kukutana kwetu.
“Wakati nipo Hospitali ya Bagamoyo na yeye akiwa pale kama muuguzi
mkuu, tulizoeana. Kuna siku aliniita kwake akasema anasafiri anaomba
nimwangalizie nyumba, nilikuwa na rafiki yangu tukawa tunalala pale
mpaka aliporudi.
“Kuzoeana kuliendelea, mwishowe tukawa wapenzi
mpaka ndoa. Nilipokumbuka hivyo tu nikagundua kuwa aliniingiza mapenzini
kwa hila au mbinu, hilo pia sikulipenda,” alisema Michael.
SIRI YA SABA Michael alisema sababu ya saba ambayo pia ilimshinikiza kuivunja ndoa hiyo ni kupwaya ndani ya nyumba.
Alisema kutokana na umri wake, ndani ya nyumba alijiona ni mtoto na si mume kama wanaume wengine walivyo.
“Hata uwezo wangu wa mawazo kwake haukuwa wa mume na mke, ni wa mtoto na mama. Kifupi haikuwa ndoa halali,” alisema.
SIKU ALIPOIVUNJA NDOA
Kijana huyo alisema ndoa yake na mheshimiwa huyo aliivunja mbele ya
Mchungaji wa Kanisa la Mikocheni ‘B’ Assemblies of God, Dk. Getrude
Rwakatare walipokwenda kusuluhishwa ili waende wakaishi kwa amani.
Alisema kabla ya usuluhishi alimfungukia mama Rwakatare kuhusu
manyanyaso anayoyapata ndani ya ndoa hiyo ndipo aliposimama na kuivua
pete kisha kuitupa chini huku akisema katu hawezi kurudi kwa mkewe huyo
na ndoa imevunjika, akaondoka zake.
ANATAKA KILIO CHAKE KIFIKE KWA JK
Kijana Michael alisema kilio chake kikubwa kwa sasa ambacho angependa
kifike hadi kwa Rais Jakaya Kikwete ni kitendo cha mkewe huyo kuzuia
vyeti vyake ambavyo vingemsaidia kutafutia kazi sehemu mbalimbali.
“Amezuia vyeti vyangu vyote, kila nikimwambia navitaka nikienda ananifanyia visa, nawaomba Watanzania wanisaidie kwa hili.
“Mimi kwa sasa nataka vyeti tu, sitaki cha ndoa wala nini? Lakini hataki kunipa,” alisema Michael.
MSIKIE MBUNGE SASA
Akijibu tuhuma hizo, Mheshimiwa Kasikila alikiri kuwa na vyeti
vinavyolalamikiwa na mumewe huyo, lakini alikanusha kwa nguvu zote juu
ya maneno kuwa yeye ameoana na mtoto mdogo, akirejea vifungu vya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vinavyomtaja mtoto kama ni mtu wa
namna gani.
Mbunge: “Mwandishi, unafahamu mtoto kwa katiba yetu ni mtu wa namna gani?”
Mwandishi: “Ni mwenye umri wa chini ya miaka kumi na nane.”
Mbunge: “Sasa Michael ni mtoto? Ana miaka 28 unamuita mtoto?”
AWAWEWESEKEA WANASIASA Alisema anajua suala hilo
lina shinikizo la kisiasa, kwani hivi karibuni baadhi ya wanasiasa
walikwenda jimboni kwake wakiwa na nakala ya gazeti moja lililoandika
habari zake na kijana huyo na kuwaambia wapigakura wake kuwa mbunge wao
ameoa kitoto, lakini wapigakura wake waliwapuuza kwa kuwaambia hilo
haliwahusu kwani wanachojua anawawakilisha vizuri bungeni.
“Kama
kweli ninyi mnampenda huyo Michael, muelekezeni sehemu sahihi ya kwenda
kupeleka madai yake. Ngoja nikupe mfano, mimi nikiwa wizara ya afya, mtu
akija na malalamiko kuhusu pembejeo za kilimo, kwa kumsaidia,
nitamuelekeza aende wizara ya kilimo, kwa kuwa pale (afya) siyo sehemu
yake, sasa nyinyi muelekezeni huyo sehemu sahihi ya kupata haki yake,
siyo huko magazetini,” alisema mama huyo.
MAMA RWAKATARE BWANA
Kwa upande wake, Mchungaji Rwakatare alipopigiwa simu kwa lengo la
kumsikia chochote kuhusu ishu hiyo, alianza kulalamikia habari
iliyoandikwa miezi miwili nyuma na kukata simu.