Mwaka uliopita ulikuwa na changamoto nyingi sana kwetu, nyinyi mlio shule na sisi tulio mtaani. Naweza kusema kuwa ni bora yenu nyie, maana bado tunawaita kula kulala, kazi kubwa ilikuwa kwetu, mwenyewe unahitaji kula, kuvaa na kulipa kodi ya nyumba ya watu na nyumbani watu wengine watano wanakusubiri!
Katika maisha, kitu kikubwa ambacho binadamu anatakiwa kuwa nacho ni malengo. Yaani ni lazima ajue anachokitaka, iwe kwa muda mfupi, wa kati au mrefu. Kwa kawaida, huwa tuna ndoto nyingi za mafanikio, lakini ni wachache ambao huzigeuza kuwa kweli.
Lakini siyo lazima kila mara kwamba utimize ndoto zako kwa asilimia zote kile unachokilenga. Kufikia hata robo ya matarajio yako ni hatua katika maisha. Hivyo usikate tamaa, kama muhula uliopita kwa mfano ulipata daraja D, ni wazi kwamba umepanda sana kama hapo kabla ulikuwa katika lile daraja ambalo sisi zamani tulikuwa tunasema Fantastic (F), sijui nyie maanko mnaliitaje siku hizi.
Kichwa cha habari hapo juu kinajieleza. Ninaposema kuigilizia, simaanishi ile tabia ya baadhi ya wanafunzi kupiga chabo kilichoandikwa na mwenzake ili na yeye aweze kukiandika katika karatasi yake wakati wa mtihani. Ninachomaanisha, ni kuiga tabia ya kujisomea ya mwenzako ili na wewe uweze kuwa bora, ikibidi zaidi yake.
Unajua, tukiwa shule kila mmoja ana usongo tofauti wa kusoma. Wapo ambao siku za nyuma niliwahi kusema, wanasoma utafikiri wametumwa na kijiji. Yaani wao wakiwa darasani, muda wote ni wao na daftari au kitabu. Wakati wengine hutumia nafasi ya kutokuwepo kwa mwalimu kwa ajili ya kupiga soga, wenyewe wapo bize na kusoma.
Utafikiri labda wako hivyo kwa sababu wapo darasani, la hasha, hata wakitoka, wakiwa nje ya darasa, mwendo ni huo huo na wakifika nyumbani ndiyo usiseme, muda wote wao ni kusoma!
Lakini kuna wengine sasa, kusoma ni mpaka awepo mwalimu karibu na anapotoka, na yeye anatoka.
Niseme kitu kimoja, kibiolojia, binadamu tunafanana kila kitu, ambacho mimi naweza kufanya hata wewe unaweza, kinachoweza kukutokea wewe, hata mimi kinaweza nitokea pia. Kwa maana hiyo, hakuna mtu mwenye akili kuliko mwenzake, isipokuwa tofauti ni jinsi gani wewe unavyoitumia akili yako kurahisisha mambo yako.
Tunawaona wenzetu na kusema, “Anko Oj ana akili sana darasani, huwezi kushindana naye”! Siyo kweli, hana akili kuliko sisi, isipokuwa yeye anatumia muda mwingi kuifikirisha akili yake, ndiyo maana muda wote inakuwa iko active. Wewe huna muda huo ndiyo maana swali au research ndogo tu inakupa taabu kweli kweli!
Ni kweli kwamba wapo baadhi yetu tunawaita genius, hawa wana vipaji maalum walivyobarikiwa na Mungu, lakini kwa jumla, kama tungetaka kujihangaisha, wote tungeweza kuwa wanazuoni wazuri sana.
Nichukue fursa hii basi kuwaasa maanko kujaribu kwa kadiri tunavyoweza, tuwe bora zaidi kitaaluma mwaka huu kuliko ilivyokuwa mwaka jana. Kama hakuna budi, siyo vibaya kama nilivyosema, kuiga baadhi ya mbinu zinazotumiwa na wenzetu ambao wanafanya vizuri darasani kuliko sisi.
Angalizo langu kwenu ni lile lile, elimu ni mkombozi wako wa uhakika kabisa. Nadhani mnawaona vijana wenzenu wanavyohangaika kutafuta maisha ya juu kwa njia za mkato, wanajikuta wanatumiwa na matajiri kusafirisha madawa ya kulevya.
Haya ni matokeo ya kushindwa kwao kuzingatia shule. Huwezi kuwa PHD Holder halafu mjinga mjinga mwenye hela zake akufuate na kukubebesha unga. Na kusoma haimaanishi hadi uwe daktari au profesa, kusoma ni kuelimika na kuelimika ni ile hali ya kujitambua, wewe ni nani, unataka nini na kwa nini!
Pigeni kitabu kwa malengo, maisha mazuri yanatusubiri!
No comments:
Post a Comment