KWELI raha jipe mwenyewe!
Usemi huo ulidhihirika wikiendi iliyopita ndani ya Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam kwenye Tamasha la Usiku wa Matumaini (Night of
Hope) ambapo wabunge mashabiki wa Yanga walikipiga na wabunge mashabiki
wa Simba na kutia fora kwa kushangiliwa wakati wa mtanange huo.
Katika mchuano huo, wabunge wa Yanga
waliwagaragaza wa Simba kwa mabao 3-2 hali iliyosababisha uwanja ulipuke
kwa kelele za kushangilia kutoka kwa mashabiki na wapenzi halisi wa
Yanga waliokuwepo uwanjani hapo.
Kama vile hiyo haitoshi, baada ya kipyenga cha mwisho, wabunge wa
Yanga walipanda mzuka na kuanza kuuzunguka uwanja wakisherehekea ushindi
wao.Wabunge waliotia fora zaidi kwa kushangilia huku wakionesha hisia kali ni Mbunge za Chalinze kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Ridhiwani Kikwete ambaye baada ya ushindi huo alikimbilia kwa mashabiki wa timu hiyo na kuvua jezi yake ya juu na kuwatupia, hali hiyo iliyomfanya kubaki tumbo wazi.
Naye Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba alikuwa sanjari na Ridhiwani ambapo yeye aliwarushia mashabiki wake ‘skafu’ aliyokuwa amejifunga shingoni, hali ambayo ilimfanya shabiki mmoja kuchomoka alikokuwa na kumfuata mheshimiwa huyo uwanjani na kuungana naye kushangilia.
Wakati huo, shabiki huyo alikuwa amevua shati na kuonekana kutoamini macho yake kwani kila wakati alikuwa akipiga magoti na kumshika miguu mheshimiwa huyo.
Matukio ya wabunge hao yaliwafurahisha mashabiki waliokuwa uwanjani hapo na shangwe kuwa kubwa kupindukia.
“Jamani sijui niseme nini, najiona kama naota hivi kwa sababu nampenda sana Mwigulu na leo nimemuona na nimemshika na kushangilia naye.
Nina raha sana na sijutii kuja kwenye tamasha hili,” alisikika akisema shabiki huyo.
Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti kwa wabunge wa Simba ambao baada ya kipigo hicho, walianza kulalamika kuwa wamehujumiwa na refarii wa mchezo huo, Othman Kazi.
Kwa upande wa muziki, mwanadada kutoka Nigeria, Yemi Alade aliwakonga nyoyo mashabiki na baadaye akakiri kwamba alifikiri itakuwa ni shoo ndogo, kumbe ni kubwa kiasi hicho, akaeleza jinsi alivyofurahi na kutamani kualikwa tena Tanzania.
No comments:
Post a Comment