Friday, April 25, 2014

Okwi: Simba SC imenipa magari sita


Okwi huyo akiondoka!
Shakoor Jongo na Musa Mateja
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Emmanuel Okwi, kwa sasa yupo nchini Uganda, aliondoka juzi Jumatano na kuzungumza na Gazeti la Championi Ijumaa pekee huku akiitaja Simba.
Okwi ambaye aligoma kucheza mechi za mwishoni mwa Ligi Kuu Bara, msimu uliomalizika hivi karibuni kutokana na kile kilichoelezwa kuwa alikuwa hajamaliziwa malipo ya usajili wake, amefunguka kuwa Simba ndiyo ambayo imemfanya kuwa vizuri kiuchumi.
Okwi akiingia ndani ya uwanja kwa ajili ya ukaguzi.
Raia huyo wa Uganda ambaye alisajiliwa ‘bure’ Étoile du Sahel ya Tunisia akitokea Simba, kabla ya baadaye kutua AS Villa ya Uganda na kisha Yanga, ameishukuru Simba kuwa ndiyo iliyochangia neema nyingi na kumfanya ajiweke vizuri kiuchumi kwa kuwekeza zaidi nchini kwao Uganda.
Okwi amesema kuwa alipokuwa Simba ni wakati ambapo aliweza kufanya mambo mengi ya kukuza pato lake ikiwemo kununua magari sita aina ya Fuso kwa ajili ya biashara, magari mengine binafsi pamoja na nyumba ya kifahari.
“Naipenda sana Tanzania na nina mambo yangu mengi tu huku,” alisema Okwi muda mfupi kabla ya kuondoka nchini, juzi, aliendelea kufunguka:
“Siyo mshahara pekee wa Simba lakini nilipokuwa pale nilikuwa nikipata vitu vingi, mfano kuna mwanachama mmoja mwanamke alinipa gari, mashabiki nao walikuwa wakinipa vitu vingi, nawashukuru sana kwa yote.”
Okwi akienda kupanda ndege.
Okwi aliongeza kuwa anarejea Uganda kwa kuwa Ligi Kuu Bara imemalizika lakini akatoa kauli kuwa atarejea baada ya wiki tatu kwa ajili ya kukamilisha mambo yake binafsi.
“Kuna vitu fulani nitakuja kuvifanya, siwezi kuvizungumza kwa kuwa ni vyangu binafsi, lakini nafikiri muda ukifika nitazungumza mengine mengi, Watanzania watajua, huu siyo wakati sahihi,” alisema Okwi.
Wakati akiondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar, Okwi alisindikizwa na watu wawili waliokuwa wamebeba mabegi yake, alipofuatwa na mwandishi wa habari (siyo wa Championi) akaweka simu sikioni na kutotaka kuzungumza chochote.
Lakini baada ya kuachwa iligundulika baadaye kuwa simu ilikuwa imezimwa na alikuwa haongei na mtu yeyote.

No comments:

Post a Comment