Wednesday, January 1, 2014

Messi aitamani Yanga


Ramadhan Singano (kulia) akijaribu kumtoka Mohamed Omar wa Jamhuri.
Na Sweetbert Lukonge
MSHAMBULIAJI wa Simba, Ramadhani Singano ‘Messi’,  amesema anatamani timu yake ikutane na Yanga kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Messi ameitabiria timu yake kufika fainali kwenye michuano hiyo inayoanza leo.
Akizungumza na Championi Jumatano, Messi ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa gumzo kubwa hapa nchini kutokana kiwango chake kuimarika kila siku alisema:
“Kikosi chetu kipo vizuri sana na safari hii lazima tuibuke mabingwa katika mashindano hayo ya Mapinduzi kwa sababu kila mtu yupo vizuri.
“Hata hivyo, ninatamani sana tukutane tena na  Yanga katika mashindano hayo na ikiwezekana iwe kwenye mchezo wa fainali na niwaonyeshe kazi wanaonibeza na kunifananisha na homa za vipindi,” anasema Messi.
Kikosi cha Simba kinaondoka leo jijini Dar es Salaam  kwenda Zanzibar tayari kushiriki mashindano hayo ambayo hufanyika kila mwaka visiwani humo na kufikia tamati Januari 9.

No comments:

Post a Comment