Friday, October 25, 2013

KIBIBI CHA MIAKA 86 CHAFANYA MAZOEZI YA KUCHANA MSAMBA

KIBIBI CHA MIAKA 86 CHAFANYA MAZOEZI YA KUCHANA MSAMBA

Ouyun, akichana msamba.
…Akiwa ameunyoosha mguu wake juu sambamba na mlingoti.
TAO OUYUN, kibibi chenye umri wa miaka 86 kutoka China, Jimbo la Zhejiang, kimeendelea kuwashangaza watu kwa kufanya mazoezi ya kuchana msamba na mengine yanayoonekana ya ajabu kwa watu wa umri wake ikiwa ni pamoja na kuunyosha mguu wake juu sambamba na mlingoti.
Kibibi huyo anafanya hivyo akiendeleza mchezo au mazoezi yanayojulikana kama Tai Chi ambayo amekuwa akiyafanya kwa miaka 36 sasa baada ya kustaafu kufanya kazi katika kiwanda cha kusokota nyuzi.

DUDE ADAIWA KUTOKA NA KIMADA WA MBUNGE

DUDE ADAIWA KUTOKA NA KIMADA WA MBUNGE

Stori: Gladness Mallya
STAA wa filamu Bongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ ameshushiwa madai mazito kuwa ameingia penzini na kimada wa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (jina tunalo), aliyetajwa kwa jina maarufu la Fetty.
Kulwa Kikumba ‘Dude’.
Kwa mujibu wa chanzo makini ambacho kiko karibu na msanii huyo, mbunge huyo kwa sasa ameshagundua kuwa Dude ana uhusiano na ‘nyumba ndogo yake’ hiyo.
Taarifa hizo zilizidi kudai kuwa, hapo awali mheshimiwa huyo ‘hakukausha nyayo’ kwa mrembo huyo lakini baada ya kugundua hali ya ‘sintofahamu’ baina ya Fetty na Dude, amesitisha ukaribu na mrembo huyo.
Baada ya kutonywa habari hizo, paparazi wetu alimtafuta Dude ili kujua ukweli wa mambo, alipopatikana alisema:
“Ni kweli hata mimi hizo habari nimezisikia kutoka kwa wasanii wenzangu na zinaniumiza sana kwani mimi najua Fetty ana bwana wake tena mheshimiwa.
Naogopa sana kutekwa, naomba kupitia gazeti hili huyo mheshimiwa aelewe kwamba mimi sina uhusiano mbaya na mwanamke wake, tumefahamiana kupitia filamu tu,” alisema Dude.
Fetty alipotafutwa kwa njia ya simu,  iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa.

AUAWA KWA KUIBA KUKU WATATU!

AUAWA KWA KUIBA KUKU WATATU!

Stori: Mwandishi wetu, Mbeya
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Frank William Shoka (30) mkazi wa Kitongoji cha Katusi, Kijiji cha Mjere, Wilaya ya Mbeya vijijini mkoni hapa ameuawa kwa tuhuma za wizi wa kuku watatu mali ya Dismas Rashid.
Kuku walioibiwa.
Akizungumzia tukio hilo, Dismas Rashidi aliyeibiwa kuku hao alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 20, mwaka huu na kuongeza kuwa marehemu alivunja banda la kuku majira ya usiku wa manani na kuchukua kuku hao wakati yeye akiwa hayupo.
Aidha, Dismas alisema baada ya kurudi nyumbani na kukuta kuku wake hawapo alianza kufuatilia na kumkuta marehemu akiwa nao katika kituo cha mabasi akitaka kuwasafirisha kwenda Mbeya na alipomuuliza juu ya kuku hao alikosa majibu wakati huo ikiwa ni saa kumi na moja alfajiri.
Hata hivyo, baada ya marehemu Shoka kushindwa kutoa maelezo sahihi juu ya kuku hao wananchi walianza kumpiga mazingira yaliyomfanya apoteze maisha.
Ndugu wakiwa na mwili wa marehemu.
NDUGU WAKAA NA MAITI KWA SAA NANE!
Hata hivyo, baada ya tukio hilo hakuna mwananchi hata mmoja aliyediriki kukaa na maiti hiyo isipokuwa ndugu wake ambao walikaa na marehemu kwa muda usiopungua saa nane.
Mwenyekiti wa kijiji cha Mjere, Mussa Tenson Mgula amesema alipata taarifa za tukio hilo kwa wananchi na alipofika alikuta mtuhumiwa ameshauawa hivyo alitoa taarifa kwa mtendaji wa kijiji  hicho, Evarist Benny ambaye alitoa taarifa Kituo cha Polisi Mbalizi majira ya saa mbili asubuhi na  Polisi walifika majira ya saa nane mchana na kuuchukua mwili wa marehemu.

MMOJA WA KUKU WALIIBIWA ATAGA
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wakati polisi wanakamilisha taratibu na kumkabidhi marehemu kwa ndugu,   mmoja kati ya kuku walioibwa alitaga yai jambo lililozua mshangao miongoni mwa mashuhuda.

KUTOKA IJUMAA:
Si jambo jema hata bkidogo kwa wananchi kujichukulia sheria mkononi, kwani sheria zipo ili zifuatwe na kama mtu amekwenda kinyume cha sheria hizo basi afikishwe kwenye vyombo vinavyohusika na sheria itachukua mkondo wake

DANGURO LA MADENTI LAFUMULIWA

DANGURO LA MADENTI LAFUMULIWA

Na Waandishi Wetu
Vijana wa Kamishina wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, CP Suleiman Kova kwa kushirikiana na Oparesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global Publishers wamefanikiwa kulifumua danguro linalodaiwa kufuga madenti wa vyuo mbalimbali jijini Dar.
Madenti hao walikamatwa mwanzoni mwa wiki hii kwenye danguro hilo lililopo ndani ya baa maarufu iliyopo maeneo ya Buguruni-Sokoni, Dar.
KERO
Awali kikosi kazi cha OFM kilipokea malalamiko kutoka kwa wazazi waishio maeneo hayo wakilalamikia ufuska wa kutisha unaofanyika kwenye danguro hilo.
Mzazi:Halooo…nazungumza na OFM?
OFM: Ndiyo…tukusaidie nini?
Mzazi: Mna habari?
OFM: Tunazo nyingi lakini ukitupatia ya kwako tutaifanyia kazi ipasavyo.
Mzazi: Tunawaamini OFM mnatisha kama njaa. Sisi ni wazazi wa hapa Buguruni-Sokoni. Kuna danguro hapa kwa kweli yanayofanyika ni aibu tupu. Tunaomba mje mjionee wenyewe mfanye kazi yenu.
OFM: Nini hasa kinafanyika?
Mzazi: Yaani vitendo vya ngono vinafanyika na sasa hivi hata kwa nje wapo watu wanafanya biashara haramu ya ngono hivyo watoto wetu wanashuhudia vitu vya ajabu na kondomu zimezagaa kila kona.
OFM: Sawa, tuachie tufanye kazi yetu.
Mzazi: Oke, lakini naomba chondechonde msinitaje wala kuonesha namba yangu kwa sababu hii ni biashara ya watu nitamwagiwa tindikali bure!
OFM: Tunaheshimu vyanzo vyetu hatuwezi kukutaja popote kwani siyo maadili ya kazi yetu.
OFM KAZINI
Kabla ya kuwataarifu polisi juu ya kero hiyo kwa wakazi wa eneo hilo, vijana wa OFM waliingia kazini ili kujikusanyia ushahidi ambapo walipofika walishuhudia vitendo hivyo vikifanyika mchana kweupe bila kujali kama kuna serikali.
Baadhi ya makachero wa OFM walijifanya wauzaji na wengine wanunuaji ambapo walijikusanyia data za kutosha huku wakiwarekodi wahusika (madenti wanaojiuza na wanaume wanaowanunua) kwa kutumia vifaa vya kazi bila wao kushtuka.
BEI
Kuhusu bei, wapo wa bei chee kuanzia buku mbili hadi tano na wa bei mbaya ambao siyo wengi, wao wakianzia dau la elfu kumi na kuendelea.
Mmoja wa vijana hao wa OFM alifanikiwa kuingia ndani baada ya kukubaliana bei na mmoja wa wauzaji ambapo alipofika na kujionea mazingira halisi aliahirisha kwa kigezo kuwa alikuwa amepokea simu ya dharura.
USHUHUDA MBAYA
Hata hivyo, alichokishuhudia ndani, anasimulia: “Nilishuhudia watu wakiwa kwenye ‘pea’ wakijiachia kwa ngono na suala la kondom ilikuwa ni uamuzi wa mtu.
“Kondom zilizotumika zilikuwa zimezagaa kila kona yaani nilihisi mwili kunisisimka na kuwaza sana juu ya janga la Ukimwi. Kwa hali ile tumekwisha.”
TAARIFA POLISI
Ili kufanikisha zoezi la kulifumua danguro hilo, OFM iliwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi na kumweleza mchezo mzima wa uchafu unaofanyika eneo hilo.
Bila kusita, kamanda huyo aliteua vijana wake kutoka Kituo Cha Buguruni ambao walitekeleza kwa kiwango cha oparesheni hiyo maalum.
Walipofika eneo la tukio, polisi hao waliwakamata wahusika wote akiwemo mmiliki wa biashara hiyo.
DENTI IFM
Wakati watuhumiwa hao wakihenyeshwa na polisi, mmoja wa madenti hao anayesoma Chuo cha IFM, Peter Davis alisema kwa upande wake aliamua kuweka makazi yake ndani ya chumba kimoja cha danguro hilo.
Katika utetezi wake, denti huyo alidai kuwa aliamua kuishi hapo kwa kuwa mazingira hayo ni mazuri kwake kwa ajili ya kujisomea.
Mwingine aliyenaswa ndani ya kiwanja hicho cha maasi ni denti aliyejitambulisha kwa jina la Mwanahamisi (hakutaja chuo) ambaye alidai kuwa tangu siku hiyo atauacha uchangudoa na kuapa kuwa akiachiwa huru ataenda kusoma kwa bidii.
Denti mwingine aliyekamatwa katika msala huo alijitambulisha kwa jina moja la Angel ambaye alidai kuwa anasoma chuo kimoja kilichopo Kariakoo, Dar na wengine hawakutaja majina zaidi ya kukiri kuwa ni wanafunzi.
MUUZA KONDOM NAYE MBARONI
Ndani ya gesti hiyo pia alinaswa njemba mmoja aliyekuwa ameweka maskani na kazi yake kubwa ilikuwa kuuza kondom kwa madenti hao ambao humwingizia kipato chapuchapu.
Hata hivyo, jamaa huyo alitiwa mbaroni kwa uchunguzi zaidi.
Mbali na oparesheni hiyo, pia polisi hao waliendeleza msako maeneo mengine ya Buguruni ambapo dadapoa kibao walikamatwa huku mmoja akiangua kilio na kutamani kujiua kuliko mumewe kujua kuwa anauza mwili.
NYUMA YA NONDO
Baada ya kuhojiwa kuhusika na biashara haramu ya ngono na kukiri, watuhumiwa hao wote waliwekwa nyuma ya nondo kwenye Kituo cha Polisi cha Buguruni na kufunguliwa jalada la kesi namba BUG/RB/13114/2013 - UMALAYA, wakisubiri sheria kuchukua mkondo wake.
WAZAZI SOMENI HAPA
Uchunguzi wa gazeti hili ulionesha kuwa madenti hao na wengine wengi jijini Dar, wamekuwa wakiaga kwao kuwa wanakwenda masomoni lakini kumbe wanaishia kwenye madanguro yaliyojazana jijini kwa ajili ya kujiuza.
Huku wazazi wakitoa fedha nyingi na huduma nyingine wakiamini watoto wao wanasoma, hali ni tofauti kwani madenti wengi wamekuwa wakiishia kwenye vitendo vya kihuni na kufeli masomo na maisha kwa jumla kisha kugeuka mzigo kwa familia.