Monday, September 2, 2013

MZEE GURUMO: DIAMOND MUNGU ATAKULIPA

MZEE GURUMO: DIAMOND MUNGU ATAKULIPA

Makala: Shakoor Jongo na Musa Mateja
Habari ya mjini wikiendi iliyopita ilikuwa ni juu ya staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kumzawadia gari nguli wa muziki wa dansi aliyestaafu muziki hivi karibuni, Mzee Muhidin Gurumo aliyekuwa akiitumikia Msondo Music Band.
Tukio hilo lililoibua maneno kibao lilijiri ndani ya Serena Hotel, Posta jijini Dar wakati Diamond au Sukari ya Warembo akizindua video ya wimbo wake mpya wa My Number One na kuhudhuriwa na raia wa kada mbalimbali wakiwemo mastaa wa muziki, filamu, wakurugenzi wa makampuni na watu wa kawaida.
Wakati Diamond akimkabidhi Mzee Gurumo ufunguo wa gari hilo aina ya Fan Cargo lenye thamani ya Sh. milioni 6 alisema:
“Nikikutajia jina la Muhidin Gurumo, basi utajua namzungumzia nani. Ni nguli wa muziki wa dansi nchini Tanzania.
“Takriban wiki imepita tangu kusikika kwa habari za kweli kuhusu kustaafu muziki kwa Mzee Gurumo, binafsi sikuwahi kukutana naye hadi leo hii nilipokutana naye kwenye uzinduzi wa video yangu.
“Nilimualika mzee huyu kwa mapenzi yote, nilisikia juzi pia akisema amekuwa akipendezwa na staili ya muziki wangu na kucheza pia, hayo ni mojawapo ya mambo yaliyonivutia kutaka kumuona mzee huyu.
“Nilipitia kwenye mitandao mingi huku ikiandikwa kuwa kutokana na kazi ya Mzee Gurumo ameweza kuwa kwenye fani zaidi ya miaka 50 lakini hakuwahi kubahatika hata kuwa na baiskeli.
“Jambo hili lilinigusa na kuniumiza moyoni, kuona nguli kama huyu wa muziki ananena vile na kuomba msaada, binafsi leo usiku nimemtunuku gari jipya mzee Gurumo kwenye uzinduzi wa video yangu.
“Nimeamua kutoa kwa moyo mmoja na kwa mapenzi yangu yote kwa mzee wangu.”
Baada ya kukabidhiwa funguo hizo na kutoa shukrani zake kwa kumuombea Diamond baraka kwa Mungu, wanahabari wetu walitaka kusikia anazungumziaje tukio hilo ambapo alisema: “Diamond Mungu atamlipa. Ni kweli nimestaafu bila baiskeli lakini yeye kanipa gari. Mungu ambariki sana.”

GARAMA
Kwa mujibu wa Diamond, video hiyo ambayo itaanza kuruka hewani leo, imetengenezwa na Ogopa Djs nchini Afrika Kusini na imegharimu dola za Kimarekani 30,000 (zaidi ya Sh. milioni 48) huku uzinduzi huo ukigharimu Sh. milioni 18. Haijawahi kutokea Bongo!

No comments:

Post a Comment