TUNAMJUA ZAIDI JAY Z, HATUMUELEWI KIDA WAZIRI
Awali ya yote, ninaomba kuomba radhi kwamba katika makala iliyopita, kwa bahati mbaya, niliandika kwa makosa kwamba Chonya alipatikana katika kitabu cha Kuli. Usahihi ni kwamba huyu jamaa alipatikana katika kitabu cha Shida na ninawashukuru wote walionikosoa!
Mimi ni shabiki wa Arsenal. Nina furaha kwamba timu yangu ilishinda mechi yake ya Jumatano dhidi ya Borussia Dortmund ya Ujerumani katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na nadhani kesho Jumapili, tunaweza kuwakalisha chini Man United pale kwao Old Trafford katika Ligi Kuu England!
Ni shabiki wa vitu vingi sana, napenda soka, muziki, filamu na kila aina ya burudani. Ninafurahishwa na baadhi ya watu katika michezo tofauti kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakifanya vizuri. Ninapopenda kitu cha Ulaya, ujue na hapa nyumbani kipo kama kile ninachokishabikia na kama sina, basi ni lazima niwe na sababu.
Nimesema ninapenda soka na ni shabiki wa Arsenal kule Ulaya, hapa nyumbani, kiasili ni shabiki wa Simba, lakini niliachana na ushabiki wa kupenda kupindukia baada ya kugundua mambo mengi ya ajabu yanayofanyika katika klabu zetu hizi mbili za Kariakoo wakati ule nikiwa Mwandishi wa michezo.
Nikakataa ushabiki huo, sisi tunalia kwa uchungu tunapofungwa, kumbe viongozi wanashangilia, wanajua nini walichofanya. Nina miaka mitatu sijakanyaga uwanjani na hata msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara sijui ulivyo!
Unajua kwa nini nimeanza hivi? Ni kwa sababu wanafunzi wengi wako hivi. Wanapenda sana vitu vya Ulaya, wenyewe wakisema mbele, lakini hawana wanachojua hapa nyumbani. Wanatumia muda mwingi kujifunza mambo ya Kimarekani kuliko kujiuliza kuhusu Tanzania na Afrika.
Leo hii ukifika katika shule zetu na vyuo, wanamuziki, wacheza filamu na wanamichezo wa nje wanafahamika zaidi kuliko watu kama hao wa hapa nyumbani. Watakuambia kuhusu Justin Bieber, kazaliwa wapi, kapiga nyimbo gani, anapenda nini na kila kinachomhusu, ikiwa ni pamoja na girlfriend wake, lakini hawana wanachojua kuhusu Abdalah Gama!
Sio vibaya kushabikia vitu vya nje, lakini basi kwa nini hatupendi kuhoji kuhusu vya kwetu? Shule ni sehemu ya kujifunza, hasa utamaduni, ujasiri na uzalendo wetu. Tunao watu waliofanya vizuri sana katika kuufikisha utamaduni wetu hapa ulipo, lakini hakuna mtu anayehangaika kutaka kuwajua.
Utashangaa wanafunzi wanaweza kumgundua mwanamuziki mkongwe wa Marekani, Jeniffer Lopez katika picha, lakini mtaani wakashindwa kumtambua Kida Waziri. Tunawapenda mastaa wetu kwa mfano akina Diamond, AY, Profesa Jay, H Baba, Ray C, Jay Dee, Linah, Barnaba na wengineo, lakini ni nadra sana kusikia wanafunzi wakiuliza kwa nini Sinza jijini Dar es Salaam kuna eneo linaitwa Kwa Remmy!
Nadhani tunakosea sana. Tunadharau sana vyetu na kuvisifu, hata kama havina ubora vile vya nje. Siyo kila kitu chetu kinafundishwa shule, vitu vingine vinataka udadisi tu wa sisi wenyewe. Kwa mfano ukiachana na akina Kinjekitile, Mkwawa, Munyigumba, Mirambo, Songea na wenzao walio katika historia, nani anatufundisha kuhusu akina Moris Nyunyusa, Mzee Makongoro na hata Mbaraka Mwishehe?
Tunatakiwa kuwa wadadisi wa kupenda sana kujua vya kwetu. Ni jambo la kushangaza kwamba kuna wazungu wanaijua nchi yetu kuliko baadhi yetu, maana sisi muda wote tupo Facebook, Twitter na Instagram ili kujua mambo ya kina Jay Z, badala ya kujiuliza kwa nini Nyerere anaonekana katika televisheni leo, miaka zaidi ya 25 baada ya kufariki kwake?