Tunaendelea na mada ya kuyachambua makundi ya wanawake na mitazamo yao kwa wanaume.
Tunaendelea kuanzia pale tulipoishia, sasa endelea...
Wale wenye vipato vidogo au wanaume wachumi, hawakubaliki kwa
wanawake wanaounda kundi hili. Mara nyingi wanawake wa kundi hili huwa
hawaivi na wanaume werevu, wenye kupenda kujiuliza mara mbilimbili kwa
kila jambo.
Kwa kawaida, wanaume werevu hutaka zaidi kuwekeza mapenzi yao kwa
wanawake wasiosukumwa na kitu ndiyo wapende. Kwa maana hiyo, mabadiliko
ya mwanamke kipindi cha fedha na pale zinapokata, huwashtua, hivyo
kuwatia kasoro.
Mara nyingi huachana, zaidi wanaume ndiyo huacha, mara chache
wanawake hukimbia. Kama wewe unadhani chako ni chenu na chake ni chenu,
utakuwa umeambulia sifuri.
Tambua kuwa chako ni chenu na chake ni chake, kama unabisha hebu
mjaribu kumuomba fedha uone kama atakupa. Akikupa lazima ataandika deni.
Na atakuwa anakudai mpaka umlipe hata kama fedha zenyewe alizitoa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.
Hata kama yeye ndiye atakuwa na
kipato kikubwa zaidi, bado hawezi kukubali kuhudumia familia wakati wewe upo.
Bora fedha zake ziende kununua nguo na kufanya mambo
mengine binafsi lakini familia lazima ihudumiwe na wewe.
TATHMINI YAO KIMAPENZIKuwa
na mwanamke wa kundi hili ni kujitafutia maradhi ya moyo. Kwa maana
tafsiri ya mapenzi ya dhati wao huichakachua kutoka kwenye uhalisia
mpaka kusomeka “fedha ndiyo mapenzi.” Hata ukiwa nazo na ukajitwisha
mzigo kumuoa na kumweka ndani, kuna siku utajuta, utalia machozi.
Vilevile yanaweza yasikutokee lakini moyoni ikawa mateso.
Umeshawahi kuona mateso ya mtu anayeumia kwa ajili ya mapenzi? Hebu omba uendelee kusimuliwa yasikukute.
Ila ukitaka nawe uwe mfano wa wanaume wanaolia mchana kweupe, jiweke kwa mwanamke
wa kundi hili halafu thubutu kuwekeza moyo wako wote. Utakonda bila kuumwa, utapoteza hamu ya kula ilhali tumboni hakuna kitu.
Leo utakuwa na fedha na unampa, atakupenda sana.
Kesho ukiishiwa utapata matokeo matatu ambayo yote ni mabaya mno kufanyiwa na umpendaye.
Mosi; anaweza kukukimbia na kutua kwa mwanaume mwingine anayeonekana ana fedha zaidi.
Hawezi kuendelea na wewe, atakwenda kuchuma kule zinapopatikana kwa
urahisi. Pili; kama mmeshaoana, atakunyanyasa ndani ya nyumba.
Anaweza kutoka nyumbani bila kukutaarifu ratiba zake, vilevile atarudi muda autakao.
Akifanya hivyo ni bora ukae kimya, kwa maana ukimuuliza au kumkosoa
unaweza kukumbana na majibu ya kuumiza sana. Usishangae akakuuliza:
“Katika wanaume na wewe umo?” Kabisa, tena atakapokuuliza hivyo atakuwa
anajiona yupo sahihi kwa asilimia 100.
Hawezi kujiona anakosea kwa sababu tafsiri yake ndiyo inamuongoza
hivyo. Anaamini ili uwe mwanaume timilifu, sharti uwe na fedha, tena
zisiishie mfukoni kwako, badala yake muwe ‘mnashea’. Zako ni zenu, zake
ni zake, tena usithubutu kufikiri zake ni zenu.
Tatu; atakuingiza kwenye madeni. Atakufanya ukope ili kumtimizia
mahitaji yake. Naye atakopa halafu atakuhimiza ulipe. Maisha yako
hayatakuwa na amani. Kwa vile muda wote anawaza fedha, atatoka nje ya
ndoa wakati wowote.
Yeyote atakayejitokeza mbele yake ambaye atamfanya awe na fedha, hatasita kumpa kilichopo ndani ya mwili wake.
Anaweza kuutoa mwili wake kwa muuza duka au genge kwa sababu hupata
mahitaji bure, hivyo kuweka kibindoni fedha ambazo humwachia za matumizi
nyumbani.
Wanawake wa kundi hili ni hatari mno, kwani unawezakupona maradhi ya
moyo kutokana na usugu wako kihisia lakini ukapata maambukizi ya
magonjwa zinaa, kwa maana hawachagui pa kujiweka.
Itaendelea wiki ijayo.